Jumatatu , 29th Dec , 2014

Jukwaa la Katiba Tanzania limeishauri serikali kusitisha zoezi la upigaji kura ya maamuzi (maoni) ya kupitisha Katiba Mpya hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ili kuleta ufumbuzi wa masuala yote tata katika Katiba Inayopendekezwa.

Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Bw. Hebron Mwakagenda

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Bw. Hebron Mwakagenda amemtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Kikwete ajipe wasaa wa kusikiliza ushauri wa wataalam nje ya serikali yake.

Amesema ushauri huo utakuwa huru na ambao utalenga kufuata maadili ya uongozi wa kisiasa na utumishi wa umma jambo ambalo wasaidizi wake wanaogopa kumshauri.

Mwakagenda Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha maoni ya ripoti kuhusu mwenendo wa mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya uliofanywa na Bunge Maalum la Katiba.

Pia ameshauri kuwa upigaji kura ya maamuzi (maoni) vema uahirishwe hadi baada ya uchaguzi wa mwaka 2015 baada ya uchaguzi mkuu na kutaka uitishwe mkutano mkuu wa kikatiba NCC ili kuleta ufumbuzi wa masuala yote tata katika katiba inayopendekezwa.

Amesema uamuzi huo nimuhimu ili upigaji kura usiwe na hofu zozote kwani kwa sasa taifa limegawanyika sana katika misingi ya kiitikadi za vyama na maslahi binafsi ya watu binafsi na vikundi vya jamii.