Jumatano , 17th Apr , 2024

Walimu katika wilaya ya Nachingwea Mkoani Lindi wametaja sababu za elimu kushuka wilayani humo kuwa ni wazazi kutowapatia watoto muda mzuri wa kujisomea, tatizo la umbali wa shule na nyumbani lakini kitendo cha wazazi kutelekeza watoto kwa wazee wasiojiweza.

Baaadhi ya Walimu wakiwa kwenye Madahalo wa Kukuza Elimu Nachingwea, Lindi.

Awali wilaya iliweza kuwa kinara kimkoa na kung’ara hadi katika ngazi ya taifa, lakini kwa sasa wilaya imeshuka kwa miaka miwili mfululizo ambapo walimu kama wazazi wanaotumia muda mwingi kukaa na wanafunzi wakisema kuwa watoto hawapo katika mazingira mazuri ya kuweza kuwasaidia kufaulu.

Wakizungumza na EATV katika mdahalo wa nini kifanyike ili kukuza elimu wilayani Nachingwea, walimu wameeleza changamoto ya watoto kutembea umbali mrefu kutoka nyumbani kuelekea shule ambapo hata wafikapo nyumbani hupambana na kazi nyingi hivyo kushindwa kupata muda mzuri wa kujisomea.

“Mazingira ya watoto sio rafiki kwa kujisomea kwasababu wengi hawalelewi na wazazi wao kwahiyo wengine wanakumbana na kazi nyingi majumbani huku pia suala la umbali likiwa ni changamoto… mwanafunzi anachoka njiani, anachelewa kufika na akifika ana njaa” Issa Selemani, Mwalimu Mpiluka Sekondari

Akizungumza kwa niaba ya Afisa Elimu wa Wilaya, Kaimu Afisa Elimu Mwalimu James Katumbi anasema kwamba kwasasa wanafanya uchunguzi katika kila kata ili kugundua changamoto mbalimbali huku wakitoa elimu kwa walimu na kuwasimamia wanayoyafundisha kama yanakwenda sambamba na muongozo.

Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mohammed Moyo amehoji kushuka huku kwa elimu ni kwanini kumetokea wakati huu ambapo serikali imejitahidi kutatua changamoto za walimu na kuwasikiliza ili kupata suluhu za changamoto ambapo pia Upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, kupitia Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Bi. Veronika Makota ametoa agizo kwa madiwani kufanya tafiti kwenye kila kata ili kupata mzizi wa tatizo.