Jumamosi , 16th Jan , 2016

Serikali imetoa siku saba kwa kiwanda cha sukari cha Mtibwa kulipa faini ya shilingi milioni 50 baada ya kudaiwa kukiuka sheria za mazingira.

Serikali imetoa siku saba kwa kiwanda cha sukari cha Mtibwa kulipa faini ya shilingi milioni 50 baada ya kudaiwa kukiuka sheria za mazingira.

Baadhiya mambo yaliyobainika ni kukosa mfumo mzuri wa kuhifadhi na kusafirisha taka ngumu na taka maji, kutohifadhi vyema kemikali zinazotumiwa na kiwanda hicho pamoja na kutumia kuni kuendesha baadhi ya mitambo yake hususani eneo la kuchemshia.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya kufanywa kwa ziara ya kushtukiza kiwandani hapo na naibu waziri wa nchi ofisi ya makamu wa Rais muungano na mazingira Luhaga Mpina, aliyeambatana na wataalamu kutoka baraza la taifa la hifadhi na usimamizi wa mazingira (NEMC).

Mh Mpina amesema tayari serikali ilishakataza viwanda kutumia kuni na magogo kuendeshea mitambo yake, huku akitoa siku 30 kwa uongozi wa kiwanda hicho cha Mtibwa kufanyia marekebisho mapungufu yote yaliyotajwa vinginevyo serikali itakifungia.

Akiwa kiwandani hapo naibu waziri Mpina amewaagiza viongozi wa mamlaka mbalimbali kuwajibika katika agizo la usafi wa mazingira kwa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi sambamba na kuwaagiza wakurugenzi wa halmashauri za wilaya kuhakikisha miti milioni 1.5 inapandwa kila mwaka.

Kaimu meneja mkuu wa kiwanda cha sukari Mtibwa Ahmad Yahya pamoja na kuridhia maagizo yaliyotolewa, ameiomba serikali kuwapunguzia faini hiyo ya shilingi milioni 50 ambayo amedai kuwa ni nyingi kwa kiwanda hicho kumudu na kueleza namna shughuli mbalimbali zinavyofanyika kiwandani hapo.