Alhamisi , 17th Aug , 2017

Mkemia Mkuu wa Serikali Prof. Samwel Manyelle amepiga marufuku wafanyabiashara wanaojishughulisha na uingizaji wa kemikali bila kibali nchini kuacha haraka kwani wanaleta changamoto na usumbufu wa usajili na hatimaye kusababisha uhakiki usio sahihi.

Akizungumza leo na wanahabari Mkemia Mkuu amesema kuanzia leo tarehe 17/8/2017 hakuna atakayeruhusiwa kujihusisha na tenda za kemikali kama hana hati ya usajili na kwamba imegundulika wafanyabiashara wengi huingiza kemikali nchini na ndipo kuomba kibali kitu ambacho ni kinyume cha sheria.

"Sheria inataka kila atakayehitaji kuingiza kemikali nchini lazima awe na hati ya usajili na kibali cha kuruhusiwa kuingiza" Mkemia Mkuu alisema

Pamoja na hayo Mkemia Mkuu ametoa ufafanuzi kuhusu maelekezo yanayotakiwa kuwekwa kwenye vifungashio vya kemikali vinavyotoka nje ya nchi.

"Kisheria Lebo inayotakiwa iwekwe kwenye kemikali toka nje iandikwe kwa lugha moja Kiswahili ama Kiingereza na siyo vinginevyo. Hakuna mzigo utakaoruhusiwa kuingizwa nchini kama maelekezo hayapo kwenye lugha hizo mbili" aliongeza

Mbali na hayo Mkemia ameziambia kampuni zote ambazo hazina usajili hazitaruhusiwa kuingiza kutumia kampuni zenye usajili.