Jumamosi , 30th Jan , 2016

Watumishi wa sekta ya afya wametakiwa kuwa wabunifu ili kuweza kutoa huduma kwa watu wote hususani wenye kipato cha juu.

Hayo yamesemwa leo na naibu waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Dkt. Hamisi Kigwangwala wakati akitembelea hospitali ya Mount Meru mkoani Arusha

Amesema hospitali zinatakiwa kusimama zenyewe kwa ukusanyaji wa mapato, hivyo upo ulazima wa kujenga au kukarabati majengo ambayo wanaweza kufanya wodi za kulipia ambazo zitakuwa zenye ubora ambao utawafanya watu wenye pesa kuja kupata huduma kwenye hospitali za umma kuliko hivi sasa wanakimbilia hospitali binafsi.

"Hii itaifanya serikali kupata pesa ambazo sehemu kubwa zitatumika kuwahudumia watu wenye kipato cha chini hospitalini hapo.

Aidha, Dkt. kigwangwala amesema licha ya serikali kupata pesa, watoa huduma pia wakiwemo madaktari, wauguzi pamoja na kada zingine kupata motisha ambazo zitawafanya kuwapa moyo wa kuwahudumia wagonjwa wa hali na Mali.

"Kama matajiri hawaji kwenye hospitali za umma, mnategemea hawa maskini watapata pesa wapi za kulipia huduma?" aliuliza.

Hatahivyo naibu waziri huyo alisema wateja wengi wanapokuja kupata huduma kwenye vituo vya huduma ya serikali, wanakata tamaa kwakuwa wanakuta hakuna watoa huduma, dawa wala vifaa tiba hivyo wanakimbilia huko pa kulipia

"Lengo letu sio kuua hospitali binafsi bali tunataka muimarishe huduma za kulipia ili tupate pesa za kuwahudumia wasio na uwezo na ninyi watoa huduma wa serikali mpate sehemu yenu ili muweze kufanya kazi kwa ufanisi.