Jumamosi , 16th Jan , 2016

Mahakama kuu kanda ya Mwanza Januari 25 mwaka huu inatarajia kutoa uamuzi mdogo wa kesi ya uchaguzi mkuu iliyofunguliwa na wakazi watatu wa jimbo la Bunda mjini dhidi ya mbunge wa jimbo hilo Mh. Esther Bulaya.

Kesi hiyo ya uchaguzi namba 1 ya mwaka 2015, inasikilizwa na Jaji wa mahakama kuu kanda ya Mwanza Mh. Gwae, huku mjibu maombi wa kwanza Mh. Esther Bulaya akitetewa na wakili Tundu Lissu, wakati msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Bunda ambaye ni mjibu maombi wa pili na mwanasheria mkuu wa serikali mjibu maombi wa tatu akitetewa na wakili Paschal Malongo.
 
Walalamikaji katika kesi hiyo ambao ni Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Ascetic Malagila wanatetewa na mawakili wawili ambao ni Costantine Mtalemwa na Denis Kahangwa.
 
Walalamikaji hao wanadai kuwa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana haukuzingatia sheria na taratibu kwani mgombea wa chama cha mapinduzi Stephen Masato Wassira aliomba kura zihesabiwe upya akakataliwa na pia hakupewa nakala ya matokeo.

Ikumbukwe kuwa Jaji Mkuu alitoa siku 90 kwa kesi zote zinazohusu uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 kukamilika ili viongozi wakaendelee na majukumu ya kutatua kero za wananchi.