Jumatatu , 26th Jan , 2015

Serikali imesema katiba pendekezwa iko kisheria na hakuna mtu yeyote anayeweza kuipinga wala kuipotosha, bali kauli ya mwisho ni ya serikali.

Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo Dkt Fenela Mukangara

Kauli hiyo imetolewa na waziri wa habari utamaduni na michezo Dkt Fenela Mukangara wakati akifungua mkutano wa wahariri wa vyombo vya habari  na mafisa habari kutoka mikoa yote nchini unaofanyika mkoani Mtwara.

Amesema  yapo maneno ya baadhi ya  wanasiasa yenye lengo la kupotosha Katiba hiyo pendekezwa,  ambayo ipo kisheria na wakati wowote itapigiwa kura na wananchi hivyo ametaka vyombo vya habari kuwa sehemu ya kuelimisha jamii na siyo kuipotosha.

Aidha ametaka wanahabari kutambua kuwa mbali na suala la katiba mwaka huu nchi inakwenda kwenye uchaguzi hivyo wasiwe sehemu ya kupotosha umma kuchagua viongozi wabovu bali, sehemu ya kuonesha kiongozi bora ni yupi.

Kwa upande wake katibu wa jukwaa la waharii Nevil Meena amesema kazi ya mwandishi ni kuripoti habari kwa kufuata misingi na sheria ya habari lengo likiwa kumlenga mwananchi ambaye ndiye mwenye maamuzi yote.

Mkutano huo umeanza leo na utadumu kwa siku Tatu pamoja na mambo mengine utatembelea hospital ya mkoa na kutoa misaada mbalimbali kwa wagonjwa.