Jumatano , 25th Mei , 2022

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro, amesema miongoni mwa matukio machache yanayowasumbua ni mauaji yanayotokana na hasira pamoja na wivu wa mapenzi na kusisitiza watu kama wamechokana ni heri wakaachana kuliko mmoja wao kumtoa uhai mwenzake.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro

Kauli hiyo ameitoa akiwa Katumba Halmashauri ya wilaya ya Nsimbo mkoani Katavi, wakati akizungumza na wananchi wa eneo hilo na kuwaomba viongozi wa dini kuendelea kutoa elimu kwa waumini wao ili kuweza kuepusha mauaji yakiwemo yale yanayotokana na ushirikina.

"Matukio machache ambayo yanatupa shida kidogo ni haya mauaji ambayo yanatokana na hasira, mwenzako kwa shida yake kaiba kuku na sheria zipo matokeo yake anapigwa kwa hasira wanamuua," amesema IGP Sirro 

Aidha IGP Sirro akaongeza tena "Mauaji yanayotokana na wivu wa mapenzi mke na mume wamekubaliana kutengeneza familia wanakuwa na ugomvi wa kawaida, baba anachukua hasira anaua mke, kama umemchoka mke au mume si mnaachana tu vizuri, na bahati nzuri kwa Afrika wanawake ni wengi kuliko wanaume kama umeona mimi nakukera niache tafuta mwingine una sababu gani ya kuondoa maisha yangu,".