Jumatatu , 20th Nov , 2017

Jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro kwa kushirikiana na madaktari wa hospital ya rufaa ya KCMC limesema linaendelea na uchunguzi wa mwili uliofukuliwa kwenye makaburi ya Karanga mji mdogo wa Himo mjini Moshi.

Mwili huo ulifukuliwa jumapili chini ya usimamaizi wa Jeshi la Polisi na kufuatia utata uliojitokeza baada ya mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Scholastica iliyopo Himo kupotea kwa siku kadhaa bila kuonekana.

“Tunaendelea na uchunguzi juu ya mwili huo na tayari kuna watu tumewakamata hivyo kila kitu kitakapokuwa sawa tutatoa ripoti kamili ya tukio hilo na wenzetu wa KCMC wanaendelea na uchunguzi wa mwili tulioufukua ili kujiridhisha kama ni wenyewe au sio”, amesema Kamishna Msaidizi wa Polisi Hamis Issa.

Humphrey Makundi, mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Scolastica anatajwa kupotea tangu Novemba 7 mwaka huu akiwa shuleni.

Kutokana na kuwepo kwa taarifa za kuokotwa kwa mwili katika mto Ghona uliopo mita 300 kutoka shule hiyo na kukosekana kwa ndugu walioutambua, mahakama ililazimu kukubali ombi la familia ya Humphrey la kufukua kaburi hilo ili kuweza kutambua kama mwili huo ni wa mtoto wao.