Ijumaa , 3rd Jun , 2016

Wafanyabiashara jijini Dar es Salaam wametakiwa kufuata miongozo inayotolewa na Jumuiya ya Wafanyabiashara pamoja na ile ya Mamlaka ya Mapato TRA, juu ya namna ya kupata mashine za risiti za kielektroniki maarufu kama mashine za EFD.

Mamlaka ya Mapato TRA imeanza kutoa mashine hizo bure kwa wafanyabiashara jijini Dar es Salaam ambapo mpaka sasa zaidi ya mashine elfu tano zimeshatolewa.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo jijini Dar es Salaam Bw. Philimini Chonde, amesema hayo leo ikiwa imepita siku moja tangu mamlaka ya mapato ianze zoezi la kugawa bure mashine hizo kwa jiji la Dar es Salaam kama njia ya kuwasaidia wafanyabiashara kuwa na kumbukumbu sahihi za mauzo katika biashara zao.

Chonde amewataka wafanyabiashara hao kwenda ofisi yoyote ya TRA ambapo watapatiwa maelekezo ya idadi na aina ya vielelezo wanavyotakiwa ili wapatiwe mashine hizo alizoeleza kuwa zitawasaidia wafanyabiashara kuendesha shughuli zao kitaalamu zaidi.

"Sisi kama jumuiya ya wafanyabiashara tunaunga mkono hatua hii ya TRA na tunawaomba wanachama wetu wajitokeze kwenda ofisi za TRA ili wapate mwongozo wa jinsi ya kupata mashine hizo," amesema Bw. Chonde.

Chonde amefafanua kuwa wakati TRA ikiendelea na utaratibu wa mawasiliano ya jinsi wafanyabiashara wanavyoweza kupata mashine hizo; wao kama Jumuiya ya Wafanyabiashara jijini Dar es Salaam wamekuwa wakiwasiliana na wanachama wao kwa njia ya mitandao ya kijamii, wakiwaelekeza vielelezo vinavyotakiwa ili kuwapunguzia usumbufu wanapokwenda ofisi za TRA.