JPM alivyotimiza ndoto ya Baba wa Taifa

Jumatano , 30th Dec , 2020

Oktoba 12, 2019, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, alitangaza rasmi kuhamia jijini Dodoma, wakati alipokuwa akijiandikisha katika daftari la orodha ya wapiga kura yeye na mke wake Mama Janeth, katika kijiji cha Chamwino mkoani Dodoma.

Kushoto ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli, na kulia ni Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere.

Rais Dkt. Magufuli, alitoa amri ya serikali kuhamia Dodoma mwezi Julai 2016, wakati alipopewa wadhifa wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), zoezi ambalo lilichukua safari ya zaidi ya miaka 40 iliyopita.

Kitendo cha Rais Dkt. Magufuli, kuamua kuihamishia serikali makao makuu ya nchi jijini Dodoma, ilikuwa ni kama ndoto ambayo ilikuwa ikingojewa kutimia kwa muda mrefu, kwani Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ndiyo ilikuwa ndoto yake kubwa ya kuihamishia serikali kwenye Makao Makuu ya nchi.

Dodoma ilitangazwa kuwa Mji Mkuu wa Tanzania mwaka 1973, lakini mnamo Aprili 26, 2018, katika maadhimisho ya miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Rais Dkt. Magufuli aliupandisha hadhi mkoa huo na kutangaza rasmi kuwa Dodoma ni Jiji.

Wakati wa maamuzi hayo Rais Dkt. Magufuli, alikuwa Rais wa kwanza kati ya marais watano waliotawala nchi hiyo, kutekeleza uhamisho wa Makao Makuu ya Tanzania kutoka Jiji la kibiashara la Dar es Salaam kwenda Dodoma.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa alihamia rasmi mji wa Dodoma septemba 30, 2016, akiongozana na mke wake na kupokelewa nyumbani kwake maeneo ya Mlimwa C, jijini humo.

Mpaka sasa tayari Wizara zote zimekwishahamia jijini Dodoma, ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Maji, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Zingine ni Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara a TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Wizara ya Ulinzi, Wizara ya Uwekezaji na nyinginezo.