Jumanne , 12th Sep , 2017

Jeshi la Polisi kupitia Msemaji wake ACP Barnabas David Mwakalukwa limekanusha taarifa zinazoendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo picha ya askari wao akihusishwa kumfuatilia Mhe. Lissu na kusema huo ni uzushi wenye lengo la kuwachafua.

Hayo yamekuja baada jana kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kusambaa picha ya moja ya askari anayedaiwa kuwa kachero wa kitengo cha Interpol kwamba yupo Jijini Nairobi nchini Kenya akifutilia taarifa ya Mhe Lissu ambaye yupo nchini humo kwa matibabu baada ya kujeruhiwa na risasi na watu wasiofahamika siku za hivi karibuni wakati alipokuwa nyumbani kwake Mkoani Dodoma 'Area D'.

"Jeshi la Polisi linapenda kukanusha taarifa hizo kuwa si za kweli na ni za uongo zenye lengo la kumchafua askari huyo na jeshi la polisi kwa ujumla. Askari huyo hayupo Nairobi kama ilivyoenezwa na picha iliyotumika ilipigwa nchini Tanzania Januari 7, 2017 kwenye sherehe ya mahafali ya mtoto wa kaka yake", amesema ACP Mwakalukwa

Pamoja na hayo, ACP Mwakalukwa ameendele kwa kusema "Jeshi la polisi linakemea vikali kitendo hicho chenye lengo la kumharibia maisha askari huyo na tunawataka wale wote waliohusika kusambaza au kutajwa katika taarifa hizo waripoti kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa ajili ya mahojiano", amesisitiza Mwakalukwa.

Kwa upande mwingine, ACP Mwakalukwa amesema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi kupitia kitengo wa makosa ya mitandao 'Cyber Crime Investigation Unit' ili liweze kuwabaini watu wote waliohusika na kusambaza kwa taarifa hizo za uongo ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.