Jaji Warioba atoa neno kuhusu Panya Magawa

Alhamisi , 19th Nov , 2020

Mkuu wa chuo kikuu cha kilimo Sokoine (SUA), Jaji Mstaafu Joseph Warioba, ameipongeza taasisi ya SUA Apopo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kufundisha Panya kutegua mabomu, hadi kupata medali ya dhahabu na kugundua magonjwa mbalimbali ya binadamu ikiwemo kifua kikuu.

Kushoto ni Panya Magawa na kulia ni Mkuu wa chuo kikuu cha kilimo Sokoine (SUA), Jaji Mstaafu Joseph Warioba.

Jaji Warioba ametoa pongezi hizo katika ziara yake aliyoifanya chuoni hapo, yenye lengo la kukagua miundombinu ya kufundishia na miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayotekelezwa chuoni hapo na kusema kuwa medali aliyopata Panya Magawa, imeleta heshima kubwa kwa nchi na kuifanya dunia itambue mchango wa watafiti waliopo Tanzania.

"Mmeiweka Tanzania katika ramani ya dunia kwamba mmeweza kukifundisha kiumbe ambacho kinafanya kazi nzuri katika mambo ya amani, nadhani hata serikali ni lazima ione fahari kwamba chuo chake kimefanya kazi hii, mnastahiri pongezi", amesema Jaji Warioba.

Panya Magawa alipewa medali hiyo ya dhahabu mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu na shirika la matibabu ya wanyama la Uingereza lisilokuwa la kiserikali (PDSA), baada ya kuweza kunusa mabomu 39 na silaha 28 ambazo hazikuweza kulipuka.