Jumatano , 6th Apr , 2016

Mahakama ya kimataifa ya makosa ya uhalifu ICC yenye makao yake makuu huko The Hague, nchini Uholanzi imetupilia mbali kesi dhidi ya Naibu Rais wa Kenya William Ruto na Mtangaz\aji wa Radio Joshua arap Sang.

William Ruto na Joshua arap Sang.

Uamuzi wa kufuta kesi hiyo umefuatia ombi la wawili hao la mwezi Oktoba mwaka jana kukubaliwa na majaji wawili kati ya watatu waliokuwa wanaounda jopo linalosikiliza kesi hiyo.

Majaji waliounga mkono ombi la kesi kufutwa na kwamba hakuna kesi ya kujibu ni Chile Eboe-Osuji na Robert Femr ambapo jaji wa tatu Olga Herrera Carbuccia alipinga lakini hoja ya wengi wape ikawezesha ombi la washtakiwa kushinda.

Majaji waliokubali ombi la kufutwa kesi walitoa sababu mbali mbali mathalani Jaji Femr alisema hakuna kesi ya kujibu kwa kuzingatia tathmini ya ushahidi wa upande wa mashtaka kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama tarehe Tatu mwezi Juni mwaka 2014.

Kwa upande wake Jaji Herrera Carbuccia, alisema uamuzi wake wa kupinga unazingatia kuwa upande wa mashtaka haujasambaratika na kuna ushahidi wa kutosha iwapo utakubalika kwa kesi kusikilizwa.

Ruto na Sang walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu nchini Kenya ikiwemo mauaji, kuwafurusha watu makwao au kuwatoa watu makwao bila hiari yao na mateso.

Makosa hayo yadaiwa kufanyika mwaka wa 2007 na 2008 wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu nchini humo.