"Hata wewe Kabudi hauwezi ukawa Rais"- Magufuli

Jumatatu , 16th Nov , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Magufuli, amesema kuwa mbunge wa jimbo la Isimani, William Lukuvi, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi, hawawezi kuwa marais kwa sababu umri wao ni mkubwa.

Kushoto ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, na kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Novemba 16, 2020, Jijini Dodoma, mara baada ya kukamilika kwa zoezi la kuapishwa kwa Mawaziri wawili pamoja na Waziri Mkuu, ambapo amesisitiza kuwa suala la uongozi siyo la kupangwa bali linakuja kwa kudra za Mungu.

"Wajumbe wa NEC walikuwa akina Lukuvi, tangu aingie mle ni mjumbe wa NEC, lakini urais hakuupata na sina uhakika kama ataupata, sasa ana miaka zaidi ya 60, yaani kwenye Kamati Kuu tuchague Rais anayenizidi umri mimi, maneno mengine yanaumiza lakini nataka niwaeleze mjitayarishe kisaikolojia kusudi msije mkapoteza hela zenu, hata wewe Prof. Kabudi hauwezi ukawa Rais, Kikwete wakati anaondoka alisema hataona Rais anayemzidi umri", amesema Rais Magufuli.

Katika hali hiyo Rais Dkt. Magufuli, amesema kuwa asilimia kubwa ya wananchi kwa sasa ni vijana na hivyo ni lazima hata Rais atakayekuja atatakiwa awe na umri mdogo, kama walivyofanya kwa upande wa Zanzibar.