Jumapili , 10th Jan , 2016

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa hatua za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba za kuimarisha huduma za afya za vijijini ni miongoni mwa utekelezaji wa shabaha ya mapinduzi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein

Dk. Shein aliyasema hayo katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora Dk. Mwinyi Makame Mwadini, mara baada ya kulifungua jengo la wagonjwa wa nje katika Hospitali ya Kivunge, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Katika hotuba hiyo, Dk. Shein alisema kuwa huduma bora za afya kwa wananchi wote bila ya ubaguzi ni miongoni mwa malengo ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 ambapo Chama cha ASP kilichoongoza Mapinduzi hayo katika manifesto yake, kiliweka bayana azma yake ya kutoa huduma za afya bure bila ya ubaguzi wakati kitakaposhika hatamu za Serikali.

Dk. Shein alisema kuwa jitihada kubwa zimefanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kipindi cha miaka 52 ya Mapinduzi katika kuimarisha huduma za afya kwa kutambua kwamba afya bora ni muhimu kwa wananchi ili waweze kuishi vyema katika kazi ya kuleta maendeleo ya nchi yao.

Alisema kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika utekelezaji wa mipango na mikakati ya kuiendeleza sekta ya afya nchini kupitia vitengo na programu mbalimbali zinazoendeshwa na serikali kwa ushirikiano na washirika wa maendeleo.

“Nyote ni mashahidi wa kuimarika kwa huduma za afya katika hospitali na vituo vytetu vyote va afya... Aidha, kuna ongezeko kubwa la vituo vya afya vya daraja mbalimbali kiasi kwamba hivi sasa wananchi wa Zanzibar hawawezi kwenda zaidi ya kilomita tano bila ya kukuta kituo cha afya”,alisema Dk. Shein.

Akieleza historia ya huduma za afya katika Mkoa wa Kaskani Unguja, Dk. Shein alisema kuwa kabla ya mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 katika mkoa huo kulikuwa na vituo viwili tu vya afya ambavyo vilikuwepo Mkokotoni na Chaani.

Alisema kuwa katika kipindi cha miaka 52 ya Mapinduzi Mkoa huo hivi sasa una vituo vya afya 26 ambapo vituo 18 ni vya daraja la kwanza na 7 ni vya daraja la pili pia, kuna hospitali ya Koteji ya Kivunge ambayo lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba ni kuipandisha daraja kuwa hospitali ya Wilaya.

Dk. Shein alisema kuwa lengo la mradi huo ulioanza mwaka 2012 ni kuziimarisha huduma za afya katika hospitali zote za Koteji ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa serikali imekusudia kuzisogeza huduma za afya kuwa karibu zaidi na wananchi ikiwa ni pamoja na huduma za upasuaji kwa kinamama wajawazito, huduma za uchunguzi kama vile za maabara, “X-ray” na “Ultra-sound”.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani za dhati kwa shirika lisilokuwa la kiserikali la Uingereza HIPZ, UNICEF na ROTARY Club kwa kuiunga mkono serikali katika lengo la kuiimarisha hospitali hiyo.

Dk. Shein alisema kuwa huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo zimeimarika sana baada ya serikali kupitia Wizara ya Afya kuongeza wafanyakazi, vifaa vya uchunguzi wa maradhi na kuongeza aina za huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwahimiza wazazi juu ya umuhimu wa kwenda kujifungulia hospitali na kuhudhuria kliniki ili kupima na kupatiwa ushauri pamoja na kuhakikisha watoto wanapelekwa vituoni kupatiwa chanjo kwa kuzingatia kampeni ya chanjo kwa watoto zinazoendeleshwa na Wizara ya Afya.

“Serikali itaendelea kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya afya kwa lengo la kuwapatia huduma bora za afya wananchi wote mjini na vijijini”,alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alitoa wito kwa wananchi wote kuendelea kusherehekea maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwa amani na utulivu.

Nae Naibu Waziri wa Wizara ya Afya Mhe. Mahmoud Thabit Kombo aliwaeleza wananchi waliohudhuria uzinduzi wa hospitali hiyo kuwa hatua hizo ni miongoni mwa ahadi za Dk. Shein kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambazo ameziahidi na sasa anaendelea kuzitekeleza huku akitoa shukurani kwa washirika wa maendeleo yakiwemo Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Mohemmed Saleh Jidawi alisema kuwa juhudi mbali mbali zinaendelea kuchukuliwa na Serikali chini ya uongozi wa Dk. Shein katika kuhakikisha Hospitali za Koteji kuwa za Wilaya na kueleza kuwa gharama za ujenzi huo ni milioni 461 chini ya ufadhili kutoka kwa Shirika la HIPZ.

Dk. Jidawi alisema kuwa lengo ni kuhakikisha hospitali hiyo inakuwa ya Wilaya na kulipongeza Shirika la HIPZ kwa kuendelea na juhudi zake katika kuiimarisha hospitali ya Kivunge kama ilivyofanya kwa hospitali ya Makunduchi.

Alisema kuwa hospitali hiyo ina uwezo wa kupokea wagonjwa 120 hadi 140 kwa siku mbapo pia hospitali hiyo itafanya kazi kwa masaa 24 huku akieleza kuwa hospitali hiyo inatumia mfumo wa kisasa wa kuwaorodhosha wagonjwa kwa njia ya Kompyuta kwa lengo la kupunguza kupotea kwa kumbukumbu.

Nao washirika wa maendeleo wakiwemo wawakilishi wa HIPZ, UNICEF, ROTARY CLUB pamoja na uongozi wa Mfuko Taifa wa Bima za Afya waliahidi kuendelea kuiunga mkono serikali katika kuimarisha zaidi huduma za afya hapa nchini ikiwa ni pamoja na kukiendeleza kituo hicho cha afya ili kitoe huduma bora kwa wananchi.

Aidha, washirika hao walieleza kuwa kituo hicho kitakuwa ni mkombozi kwa akina mama na kutoa shukurani kwa mashirikiano wanayoyapata kutoka kwa uongozi wa Wizara hiyo.

Viongozi mbalimbali wa vyama na serikali pamoja na mamia ya wananchi walijitokeza katika hafla hiyo.