Alhamisi , 25th Aug , 2016

Mkuu wa wilaya ya Manyoni mh. Geofrey Mwambe, amesema kwa kushirikiana na wakuu wenzake wa wilaya jirani, watahakikisha wanapambana kukomesha ujangili kwa lengo la kulinda na kuhifadhi rasilimali adimu za wanyama na misitu katika maeneo yao.

Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Geofrey Mwambe (mwenye suti nyeusi ya mikono mirefu) akishuhudia kufungwa kwa mafunzo ya kudhibiti ujangili unaotokea kwenye misitu ya Hifadhi ya Rungwa-Kizigo-Muhesi wilayani Manyoni, mafunzo yaliyotolewa na wakufunzi kutoka North Carolina nchini Marekani.

Wilaya hizo alizopakana nazo ni pamoja na Chunya, Iringa, Sikonge na Songwe,

Mheshimiwa Mwambe amesema hayo wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya kudhibiti ujangili unaotokea kwenye misitu ya Hifadhi ya Rungwa-Kizigo-Muhesi wilayani Manyoni, mafunzo yaliyotolewa na wakufunzi kutoka North Carolina nchini Marekani, hafla iliyohudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Jenerali Gaudense Milanzi na Balozi wa Marekani nchini Mark Childress.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida mhandisi Mathew Mtigumwe; Mwambe amesema kama serikali wamedhamiria kupambana na majangili kokote walipo ambapo ametoa wito kwa wanaojihusisha na biashara hiyo kuacha mara moja na kujielekeza kwenye shughuli halali za kujipatia kipato.

Tangu ateuliwe kuwa mkuu wa wilaya ya Manyoni, DC Mwambe amepata sifa kemkem kutoka kwa wakazi wa wilaya hiyo kwa jinsi alivyo mbunifu wa miradi mbalimbali yenye lengo la kuinua hali ya maisha ya wananchi wa Manyoni.

Sehemu ya ubunifu huo ni uanzishwaji wa mfuko wa maendeleo wa wilaya ya Manyoni ujulikanao kama Manyoni Development Fund pamoja na mpango wa usimamizi bora wa madawati yaliyotolewa na serikali kwa ajili ya shule za msingi na sekondari.