Jumanne , 15th Mar , 2016

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Fadhili Nkulu ameibiwa kiasi cha shilingi milioni 10 na wezi wa mtandao ambao waliteka mawasiliano yake ya simu za mkononi kwa muda wa saa 3 na kutumia namba hizo kuomba fedha kwa watu wa kawaida.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha Fadhili Nkulu.

Akizungumza na waandishi wa Habari Ofisini kwake ,Nkulu amesema kuwa jana majira ya saa 10:00 alasiri simu zake zilikua hazipatikani hewani mpaka majira ya saa 3:00 usiku ndipo aliposhtuka na kuanza kufuatilia na kugundua kuwa mawasiliano yake yalitekwa kwa muda.

Mkuu huyo wa Wilaya amelaani vitendo vya wizi wa mtandao vinavyofanywa na watu wenye nia ovu huku akiwataka wananchi na wamiliki wa makampuni ya simu kuwa makini juu ya wizi huo wa kimtandao ambao umeshamiri miaka ya hivi karibuni.

Msaidizi wa Mkuu wa Mkoa Yoitham Ndembeka ambaye alitumiwa ujumbe wa kumtaka atume fedha kupitia namba ya mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa baada ya kusumbuliwa na matapeli hao ambao hawakutaka kupokea simu aliamua kuachana nao huku akitafuta namna ya kuonana ana kwa ana na Mkuu huyo wa Wilaya.

Wizi wa mitandao umeshamiri na kushika kasi hasa katika kipindi hiki ambacho teknolojia imekua kwa kiasi kikubwa ,hivyo makapuni ya simu,mamlaka za kusimamia teknolojia ya mawasiliano TCRA pamoja na polisi wanapaswa kuchukua hatua kupambana na uhalifu huo.