Alhamisi , 19th Nov , 2020

Katika kuadhimisha kilele cha Wiki ya Choo Duniani na Unawaji wa Mikono jamii imeshauriwa kujali afya na mazingira ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa maji safi na salama na matumizi bora ya choo ili kuepukana na maradhi.

Mkuu wa wilaya ya Ilala, Ng'wilabuzu Ludigija.

Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam katika maadhimisho hayo Mkuu wa wilaya ya Ilala Ng'wilabuzu Ludigija, amesema pamoja na jitihada zilizofanywa na Manispaa ya Ilala na wadau wamaendeleo ya afya bado kunachangamoto ya unawaji mikono ambapo mwitikio umekuwa mdogo na kuwataka walimu kuendelea na zoezi la unawaji wa mikono mashuleni.

Kwa upande wake Meneja Miradi ya Mazingira na Usafi wa Afya (AMREF), Mhandisi Mtuli James, amesema bado kuna changamoto ya elimu juu ya choo bora kwa jamii hivyo wana mkakati wa kuendeleza elimu ya matumizi ya vyoo bora ambapo mpaka sasa wamefikia watu 10,000 kwa kaya na watu wasiopungua 60,000.

Naye Balozi wa Kampeni ya Nyumba ni Choo, Mrisho Mpoto, amesema malengo ya kufanya madhimisho hayo ni kuweza kuwafikia watu wengi na kuwapa elimu ambapo amewapongeza Watanzania kwa kuwa na mwamko choo bora na kunawa mikono ili kuondokana na tamaduni za kizamani na kuleta matokeo chanya.