Dawa za kuvutia wanaume wapewe ambao hawajaolewa

Jumamosi , 6th Feb , 2021

Wazazi ambao wanawapa dawa za mvuto na nyota watoto wadogo ili wapendwe, wametakiwa kuwapa dawa hizo watu wazima ambao hawajaolewa badala ya kuharibu ndoto za watoto kwa kuwakatisha masomo, hali inayopelekea kukumbana na mimba za utotoni.

Josephine Ngoda

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa asasi ya wanawake laki moja Josephine Ngoda, wakati akizungumza na wanawake wa mkoa wa Shinyanga kwenye uzinduzi wa asasi hiyo,ambapo amesema mkoa huo umekuwa na matukio mengi ya ukatili wa kijinsia vikiwemo vipigo, ubakaji wa watoto na kulawiti vitendo ambavyo vinasikitisha na kuumiza jamii.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack, akizindua asasi hiyo inayojihusisha na kupinga ukatili wa kijinsia na umaskini, amewataka wanawake kuvunja ukimya na kuacha kufumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia wanavyofanyiwa.

Aidha RC Telack amewataka wanawake kuacha kuwalaza chumba kimoja watoto wa kike na wakiume pamoja na kuwalaza na wageni kwani ni hatari na ni chanzo cha watoto wa kike kuanza kufanyiwa vitendo vya ukatili na kupewa maneno ya vitisho kwamba wasiseme.