Jumatano , 30th Dec , 2020

Machi 16, 2020, Tanzania ilithibitisha kisa cha kwanza cha mgonjwa wa Corona, taarifa ambayo ilitolewa na Waziri wa Afya wa wakati huo Ummy Mwalimu, ambaye alisema kuwa mgonjwa ni mwanamke raia wa Tanzania aliyewasili nchini Machi 15 kupitia uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanajaro.

Kushoto ni Rais Dkt. John Magufuli, na kulia ni kipimo cha COVID-19

Taarifa ya Waziri Ummy, ilieleza kuwa mgonjwa huyo aliwasili na ndege ya shirika la Rwanda akitokea nchini Ubelgiji, ikiwa ni moja ya Taifa ambalo lilikuwa limeathirika na virusi hivyo kwa kiasi kikubwa.

Mara baada ya mgonjwa wa kwanza kuthibitika nchini, Machi 17, 2020, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alitangaza kufunga shule kwa muda wa siku 30, pamoja na kuzuia mikusanyiko mbalimbali ikiwemo matamasha na michezo, mikutano mbalimbali ikiwemo ya shughuli za kisiasa, jambo ambalo lilikuwa ni kama tahadhari za kujikinga na kusambaa kwa maambukizi ya virusi hivyo.

Mbali na serikali kuchukua hatua hizo, Serikali pia ilijipanga kwa uhakika kwa kuweka mazingira ya kukabiliana na ugonjwa huo ikiwemo kutenga hospitali maalum za Mloganzila ya Dar es Salaam, kituo cha Buswelu (Mwanza) na Hospitali ya Mawenzi (Kilimanjaro), Mnazi Mmoja (Zanzibar) na ChakeChake (Pemba) kwa ajili ya kutoa huduma kwa waathirika wa ugonjwe huo.

Safari ya kuchukua tahadhari ikaanza rasmi kwa Watanzania, ikiwemo uvaaji wa barakoa, kuepuka mikusanyiko, unawaji wa mikono, utumiaji wa vitakasa mikono huku nguvu kubwa ikiwekezwa kwenye maombi.

Aprili 16, 2020, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa twitter, Rais Dkt. Magufuli, aliwataka Watanzania kutenga muda wa siku tatu kwa ajili ya dua na sala zao kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuliponya Taifa na janga hilo ambalo hata sasa bado linasumbua Mataifa mengi Duniani.

Aprili 22, 2020, Rais Magufuli, aliwahutubia Watanzania akiwa Chato Geita, na kuwatoa hofu waliyonayo kuhusu ugonjwa huo, ambapo alizuia masuala ya 'lockdown' kama ambavyo watu wengi walipendekeza kwa kipindi hicho na kueleza kuwa siyo wote wanaofariki dunia ni kutokana na ugonjwa bali wengine wanafariki kutokana na hofu waliyonayo.

Kauli hiyo ya Rais Dkt. Magufuli, iliamsha matumaini ya Watanzania yaliyokuwa yamelala, ilirejesha tumaini jipya na mwangaza kwenye nyuso za watu wengi waliokuwa hawana matumaini, hii yote ni kulingana na takwimu za maambukizi na vifo vya watu kutoka katika maeneo mbalimbali Duniani.

Mbali na Dkt. Rais Magufuli, kuzuia 'lockdown' kama ambavyo mataifa mbalimbali Duniani yalikuwa yamekwishachukua hatua za kuwafungia wananchi wake ndani, yeye pia alisisitiza suala la matumizi ya tiba mbadala ikiwemo kujifukiza na kupiga nyungu.

Mpaka sasa Watanzania wengi na mataifa mengi Duniani, wamekuwa wakimpongeza Rais Magufuli, kwa kauli yake ya kishujaa kwani yeye aliamua kuwa mstari wa mbele katika mapambano hayo licha ya wananchi wake kuendelea kuchukua tahadhari za ugonjwa huo, lakini kauli yake moja tu ndiyo ilikuwa tiba na kupelekea mpaka sasa Tanzania haijatangaza tena kisa kipya cha mgonjwa wa COVID-19.

Ugonjwa wa Virusi vya Corona (COVID-19), ulianzia nchini China mwishoni mwa mwaka 2019, na kusambaa Mataifa mbalimbali Duniani.