Akiongea na East Africa Radio leo Katibu Mwenezi wa CHAUMA Eugine Kabendera amesema walituma barua mapema za kutokushiriki uchaguzi huo wa marudio kwa tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC), kwa Rais Magufuli na kwa Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein.
Amesema walituma pia katika ofisi zote za ubalozi nchini hivyo wanaamini kuwa uamuzi wao ni sahihi na kuamini kuwa mshindi halali ni yule aliechaguliwa tarehe 25 mwezi Oktoba na siyo kurudiwa kwa uchaguzi.
Aidha ameongeza kuwa katika nchi inayokuwa na vyama vingi ni lazima kuwepo na chama kimoja ambacho kitashinda hivyo wanasiasa wawe wanajiandaa kisaikolojia kushinda au kushindwa ili kuepusha migogoro kama hii ambayo inaonekana kusababaishwa na baadhi ya viongozi kukataa kuachia madaraka.
Kuhusiana na suala la uchaguzi wa Meya wa jiji la Dar es salaam amesema mambo yanayoendelea hivi sasa ni kufifisha demokrasia hivyo anaishauri serikali kuingilia kati suala hili kwani linaharibu taswira ya nchi yetu nje ya mipaka ya Tanzania.