Ijumaa , 30th Oct , 2020

Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Nkasi Kaskazini, amemtangaza Aida Khenani, wa CHADEMA kuwa ndiye mbunge wa jimbo hilo baada ya kupata kura 21,226, na kumshinda Ally Keissy wa CCM aliyepata kura 19,972 na hivyo yeye kuwa mgombea wa kwanza kukitetea chama chake katika nafasi hiyo.

Aida Khenani, mbunge mteule wa jimbo la Nkasi Kaskazini kupitia CHADEMA.

Aida Khenani kabla ya Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuvunjwa, alikuwa ni Mbunge wa Viti Maalum kuanzia mwaka 2015 hadi 2020 kupitia chama chake cha CHADEMA.

Mbali na CHADEMA kupata mtetezi wake wa kwanza Bungeni mpaka sasa tangu matokeo ya uchaguzi yaanze kutangazwa, chama cha CUF pia kinaye mwakilishi kutoka jimbo la Mtwara Vijijini, ambaye ni Shamsia Mtamba, aliyepata kura 26,262, na kumshinda aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia CCM Hawa Ghasia aliyepata kura 18,505.

Katika matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28 mwaka huu, mpaka sasa vyama vya upinzani yaani CHADEMA na kile cha CUF kina wawakilishi wawili pekee wa ubunge ambao tayari wamekwishatangazwa, huku wabunge wengine wa vyama vya upinzani wakishindwa kutetea majimbo yao ambayo kwa asilimia kubwa yamechukuliwa na CCM.