Jumatatu , 23rd Mei , 2022

Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimetaja mambo kumi waliyoyafikisha katika kikao walichoshiriki wiki iliyopita kilichoongozwa na Rais Samia Suluhu na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM na CHADEMA.

Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika

Akizungumza na wanahabari leo Mei 23/2022 Katibu Mkuu wa CHADEMA John Mnyika amesema miongoni mwa ajenda hizo ni Mchakato wa Katiba mpya, Madhara ya ukiukwaji wa haki kwa miaka sita iliyopita na kupendekeza kuundwa kwa tume ya ukweli na upatanishi.

Mengine ni kushughulikiwa kwa madhara yaliyotokana na uchaguzi wa 2020, uhuru wa vyama vya siasa kufanya shughuli zake, kufutwa kwa kesi zenye muelekeo wa kisiasa, kurekebisha sheria kandamizi, kushughilikia masuala yanayohusu viongozi, wanachama na watu walioshambuliwa, kupotea au kuuawa kwa sababu za kisiasa.

Aidha ametaja masuala mengine kuwa ni sakata la wabunge 19 wa viti maalumu waliofukuzwa CHADEMA, hakikisho la usalama kwa viongozi waliopo nje kwa sababu za kisiasa, kuvurugwa kwa kambi ya upinzani bungeni, pamoja na madhara yaliyowakumba watu mbalimbali kwa sababu ya kukandamizwa kwa haki na Demokrasia.

Mnyika amewataka wanachama wa CHADEMA kuwa watulivu katika kipindi hiki cha mazungumzo hayo huku akisema taarifa za kinachoendelea kitatolewa kupitia vikao halali vya chama hicho