Jumatatu , 20th Apr , 2015

Wakaguzi wa hesabu za serikali nchini Tanzania wametakiwa kufanya ukaguzi kwa kushirikisha masuala ya kisheria ili kupata ushahidi wenye nguvu ambao ukifikishwa mahakamani utatoa matokeo mazuri ya ushindi.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali nchini Tanzania, Profesa Mussa Assad.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Musa Juma Assad, ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam leo, katika uzinduzi wa mafunzo ya wakaguzi wa hesabu kwa nchi za Afrika zinazungumza lugha ya kiingereza.

Profesa Assad amewaambia watalaam hao kwamba ili uchunguzi wao kwa taasisi za serikali uweze kufanikiwa ni lazima uangalie masuala muhimu ya kisheria kwa kuwa kipengele hicho kikiachwa watuhumiwa watashindwa ama kesi zao zitafutwa zitakapofikishwa mahakamani.

Ametolea mfano wa kesi moja hapa nchini ambayo hata hivyo hakuitaja kwamba mshtakiwa alihukumiwa na mahakama kwenda jela, lakini kwa bahati nzuri alitolewa kwa msamaha wa Rais na alipoenda kukata rufaa mahakama kuu kesi yake ilifutwa.

Amesema ofisi yake ina kitengo cha sheria ambacho kilianzishwa mwaka 2010 ambacho kinatoa ushauri wa kisheria pale wanapoenda kufanya uchunguzi wa matumzi mabaya ya fedha za serikali katika mashirika na taasisi za serikali.

Ameongeza kuwa kitengo hicho kinahakikisha ofisi yake inatoa tafsiri ya kisheria katika sekta husika inayokaguliwa na CAG pamoja na kuandaa mafunzo katika mambo ya ukaguzi wa fedha.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga amewaambia washiriki hao kuwa, masuala ya kisheria ni muhimu na yanahusiana na shughuli za ukaguzi wa hesabu za serikali ili kuupa uzito ushahidi utakaowasilishwa mahakamani.

Amesema kuna haja ya wanasheria kwa wanaoshirikiana na CAG, kujiangalia vizuri ili kuhakikisha vitu vinavyochunguzwa vinapata uzito ili visitupwe mahakamani.

Amefafanua kuwa masuala ya ukaguzi wa hesabu za serikali unahusisha taasisi nyingi na kwamba uzingatiaji wa kisheria ni muhimu vinginevyo mahakama itatupa ushahidi kama haukuzingatia masuaa ya kisheria.

Washiriki hao wanatoka nchi za Kenya, Uganda, Lesotho, Sudan na wenyeji Tanzania na wanahudhuria mafunzo ya siku mbili yaliyoanza jana jijini Dar es Salaam.