Ijumaa , 22nd Aug , 2014

Ofisi ya mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali imebaini udhaifu mkubwa wa baadhi ya halmashauri za wilaya nchini kuwa zimekua zikihujumiwa na kushindwa kusimamia ukusanyaji wa mapato.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG Ludovick Utouh.

Mapato hayo ni yale yanayokusanywa kupitia kwa mawakala walioingia nao mikataba hatua inayofanya halmashauri hizo kushindwa kujiendesha.

Aaizungumza na EATV Jijini Tanga jana, Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Ludovick Utoh amesema udhaifu huo umetokana na sera ya serikali kuu kukubali kulipia gharama za uendeshaji wa halmashauri nchini hatua ambayo imesababisha baadhi ya halmashauri hizo kushindwa kutilia mkazo suala suala zima la ukusanyaji wa mapato.

Bw. Utoh ameongeza kuwa utafiti uliofanywa na ofisi yake umebaini kuwa baadhi ya mawakala wanaokusanya ushuru katika maeneo ya wazi ikiwemo vituo vya mabasi,masoko na vyanzo vingine vya mapato kiwango kinachopelekwa halmashauri ni asiliamia 30 tu na asilimia 70 inabaki kwa wakala.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa umma Bw. George Yambesi amesema ofisi yake inafanya jitihada za kuhakikisha kila halmashauri inabaini vyanzo vyake vya mapato na kuvipa vipaumbele ili viweze kutumika kwa ajili ya maendeleo ya maeneo yao na taifa kwa ujumla.