Jumanne , 23rd Jun , 2015

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo limepitisha Bajeti ya Serikali ya trilion 22.4 kwa mwaka 2015/2016 iliyowasilisha june 11 na Waziri wa Fedha Mh. Saada Mkuya Salum ambayo imefanyiwa marekebisho kadhaa.

Waziri wa Fedha Mh. Saada Mkuya Salum akijibu hoja za Wabunge kuhusu Wizara ya Fedha.

Akijibu hoja za Wabunge kuhusu bajeti hiyo Waziri Mkuya amesema kuwa moja ya maeneo yaliyofanyiwa marekebisho ni Pensheni ya Wazee wastaafu wa Utumishi wa Umma kwa kupandisha hadi shilingi laki moja kutoka elfu 85 iliyokuwa imetajwa awali kupandishwa kutoka sh. elfu 50 ya awali.

Waziri Mkuya ameongeza kuwa kutokana na ufisadi iliopelekea kupotea zaidi ya shilingi. Bilioni 6 za Wazee wote wanaokadiriwa kuwa milioni 1.2, serikali imeandaa mfumo maalum wa kuwatambua wazee hao ili waweze kufikishiwa pensheni zao kwa wakati.

Kuhusu tozo ya mafuta iliyokuwa ikilalamikiwa na wabunge wengi Mkuya amesema kuwa tozo hiyo iliyoongezeka kutoka shilingi 50 hadi shilingi 100 itabaki palepale ili kusukuma kasi ya maendeleo hasa vijijini.

Mkuya amesema kuwa kutokana na tozo hiyo, serikali inalenga kukusanya kiasi cha shilingi bilion 276 ambacho kati yake bilion 90 zitatumika kwa ajili mfuko wa maji ili kutatua kero ya upatikanaji maji na shilingi bilioni 186 itatumika kwa ajili ya kupeleka umeme vijijini.

Aidha Mh. Mkuya amewataka wananchi waendelea kuchangia maendeleo ya nchi kupitia tozo ya mafuta na kukataa kushashiwa kugoma kuchangia maendeleo kwa njia za uhakika kama hizo

Bajeti hiyo imepitishwa na jumla ya wabunge 294 waliokuwemo bungeni kwa njia ya kuitwa jina na kukubali au kukataa bajeti.

Kati ya wabunge hao, 219 sawa na asilimia 83 ya wabunge waliokuwemo akiwemo mbunge wa Maswa Magharibi John Shibuda (CHADEMA) na John Cheyo (UDP) wameipigia kura ya NDIYO kuikubali bajeti hiyo, na wabunge 74 akiwemo Augustin Mrema mbunge wa Vunjo wameipigia kura ya HAPANA kuikataa huku mbunge mmoja akigoma kufanya maamuzi.