Jumatatu , 20th Mar , 2017

Benki ya Dunia inatarajia kutoa kiasi cha Shilingi Trilioni 1.7 kwa Tanzania kwa ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali ya huduma za jamii ikiwemo elimu.

Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Jim Yong Kim

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Jim Yong Kim alipotembelea Shule ya Msingi ya Zanaki ya Jijini Dar es Salaam, ambayo ni moja kati ya shule zinazonufaika na fedha za Benki ya Dunia.

Amesema msaada huo ni mkopo wenye lengo la kuisaidia Tanzania katika uboreshaji wa miundominu ya elimu hasa maeneo ya vijiji yasiyofikiwa kwa urahisi na huduma hiyo kutokana na miundombinu mibovu.

Dkt. Kim amesema Benki ya Dunia itaendelea kuisaidia Tanzania kwakuwa ni moja ya nchi inayotumia vizuri fedha inazozitoa na kujiletea maendeleo kwa wakati na kuzitaka nchi nyingine zijifunze matumizi mazuri ya fedha za misaada kutoka kwa Watanzania.

Akizungumza wakati wa makubaliano hayo Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philipo Mpango amesema serikali itahakikisha fedha hizo zinaenda kuboresha miundombinu ya elimu ili kuhakikisha taifa linapiga hatua katika sekta ya elimu na kufikia malengo ya milenia katika sekta hiyo waliojiwekea.

Prof. Joyce Ndalichako - Waziri wa Elimu

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema wana mpango wa kuendelea kujenga zaidi shule kwa kuwa elimu ya bure imeongeza idadi ya wanafunzi hivyo bado kuna changamoto ya vyumba vya madarasa.