Jumatatu , 15th Sep , 2014

Waziri Mkuu wa Nchini Tanzania Mizengo Pinda amewataka Wakala wa Wakulima Wadogo wa Chai pamoja na Bodi ya Chai nchini waangalie uwezekano wa kuunda timu ya watu wawili au watatu itakayosimamia mwenendo wa kiwanda cha chai Mponde,kilichopo lushoto.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda.

Waziri Mkuu alipokea taarifa fupi ya mgogoro wa kiwanda hicho kabla ya kuzungumza na wakulima, wadau wa zao la chai na viongozi wa mkoa na wizara kadhaa kwenye mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga.

Waziri Mkuu amesema timu hiyo kwa kushirikiana na mwekezaji hawana budi kuandaa mpango-kazi wa miaka miwili hadi mitatu wa kufufua kiwanda ili uzalishaji wa chai ufikie pazuri.

Amesema ili kuweza kusonga mbele, itabidi Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) aende kufanya ukaguzi kwenye kiwanda hicho ili kuweza kutoa picha halisi ya kiwanda hicho kwa sababu Serikali ina hisa.

Kiwanda cha Chai cha Mponde kinamilikiwa na Chama cha Wakulima wa Chai cha UTEGA (Usambara Tea Growers Association) ambacho kilitafuta mwekezaji ambayo ni Kampuni ya Chai ya Lushoto (Lushoto Tea Company). Wakulima wa Chai walikifungia kiwanda hicho kisifanye kazi kwa madai kuwa walikuwa hawalipwi malipo kwa wakati, wamiliki kutumia lugha chafu.