Jumamosi , 18th Oct , 2014

Nchi za Afrika pamoja na Jumuiya ya Kimataifa zimelaumiwa kwa kuchelewa kuchukua hatua za kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa hatari wa Ebola ambao umezikumba na kuziathiri nchi za Liberia, Guinea na Sierra Leone.

Lawama hizo zimetolewa leo jijini Dar es Salaam na wadau mbalimbali wa tasnia ya habari, ambao wameshiriki kongamano kuhusu ugonjwa wa ebola, kongamano lililoandaliwa na kampuni ya vinywaji baridi ya Coca Cola, kama sehemu ya shughuli za kuelekea fainali za Tuzo ya Mwandishi Bora Barani Afrika za CNN Multichoice African Journalist Awards zinazofanyika jijini Dar es Salaam muda mfupi kuanzia hivi sasa.

Kwa mujibu wa wadau hao, tangu mlipuko wa ugonjwa huo ulipotokea Disemba mwaka jana, hakuna juhudi zozote za pamoja zilizochukuliwa kuudhibiti usilete madhara zaidi kwani ilichukua miezi sita kwa shirika la Afya Ulimwenguni kuanza kuchukua hatua za kukabiliana nao.

Aidha, wadau hao pia wamesikitishwa na namna waandishi wa habari walivyochelewa kuchukua jukumu la kuelimisha kuhusu namna ya kukabiliana na ugonjwa huo, hatua wanayosema ingeweza kuzuia vifo takribani 4500 kati ya watu zaidi ya elfu tisa waliothibitika kuambukizwa na kuugua ugonjwa huo.

Aidha, mmoja wa waandishi wa habari waandamizi barani Afrika Bw. Amadou Mahtar Ba, amezitaka nchi za Afrika hasa zile zilizo jirani na nchi zenye ugonjwa huo kujiandaa na kile alichokiita kuwa ni wakimbizi wa ebola, ambao watatokana na makundi ya watu wanaokimbia kunusuru maisha yao kutokana na hatari ya ugonjwa wa ebola.