2020 Halima Mdee alivyoshangaza

Alhamisi , 31st Dec , 2020

Wabunge wateule wa viti maalum kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA Halima Mdee, Novemba 24, 2020, walikula kiapo cha nafasi hiyo katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

Halima Mdee, mbunge wa Viti Maalum, na aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo la Kawe.

Zoezi la uapisho wa wabunge hao liliongozwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai.

Akizungumza mara baada ya kula kiapo, Halima Mdee alisema kuwa, "Nikishukuru chama changu cha CHADEMA kikiongozwa na Mwenyekiti wetu Freeman Mbowe, ambao kupitia wao sisi tumepata nafasi ya kukiwakilisha chama chetu, viti hivi siyo hisani ila ni sehemu ya ushindi mkubwa ambao chama chetu kilipata".

Mara baada ya wabunge hao kula kiapo, kwenye mitandao ya kijamii watu wengi walionekana kumtupia lawama aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kawe, Halima Mdee, tofauti na wale wenzake 18, kwani watu wengi waliamini msimamo wake kwani hata baada ya kushindwa katika uchaguzi huo alidai kuwa hawezi kula kiapo cha ubunge wa viti maalum kwa madai ya kwamba uchaguzi haukuwa huru.

Halima Mdee na wenzake 18 wakiwa kwenye picha ya pamoja na Spika wa Bunge na Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai, baada ya kula kiapo.

Baada ya taarifa za wabunge hao 19 kusambaa, baadaye viongozi wakuu wa chama cha CHADEMA walijitokeza mbele ya vyombo vya habari na kusema kuwa, akina Halima Mdee na wenzake ni wasaliti na waongo, kwani kiapo walichoapa ni batili na wala hakikuwa na baraka za viongozi wa chama kama ambavyo mwanzo Halima alidai.

Baadaye Kamati Kuu ya CHADEMA iliketi jijini Dar es Salaam, na kufikia maamuzi ya kuwafukuza uanachama wabunge hao 19, kwani hata baada ya kutumiwa barua ya wito, hawakuhudhuria kikao hicho kwa kile walichodai kwamba wote kwa pamoja wana dharura na kuomba kikao kisogezwe mbele jambo ambalo halikuwezekana.

Mara baada ya madai hayo, Halima Mdee na wenzake 19, walijitokeza nao mbele ya vyombo vya habari na kudai kuwa, licha ya kwamba wamefukuzwa uanachama lakini wao wako tayari kuwa wanachama wa hiyari na kwamba hawawezi kuongea mambo mengi hadharani bali watarudi ndani ya chama chao kuyajenga.

Mbali na maamuzi ya chama chao cha CHADEMA, lakini Spika wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, alisema kuwa wabunge wote aliwaapisha anawatambua na kudai kuwa chama cha CHADEMA, kimekuwa na tabia ya kuwakandamiza wanawake na kukitaka kuacha hiyo tabia.

Wabunge waliokula kiapo hicho na kufukuzwa uanachama ni 19, akiwemo Ester Bulaya, Salome Makamba, Grace Tendega, Kunti Majala, Esther Matiko, Halima Mdee, Cecilia Paresso, Agnesta Lambati, Nusrat Hanje, Jesca Kishoa, Tunza Malapo, Konchester Leonce Rwamlaza.