Zanzibar ilipofikia kwenye Mapinduzi

Jumanne , 12th Jan , 2021

Usultani ulianzishwa rasmi Zanzibar wakati Sultani Sayyid Said alipoamua kuhamisha makao makuu yake kutoka Maskat (Omani) kwenda Unguja.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Hassan Mwinyi.

Sayyid Said alikuwa Sultani wa Omani tangu mwaka 1804. Aliimarisha utawala wa Omani juu ya pwani ya Afrika ya Mashariki.

Mwaka 1829 alifaulu kuteka Mombasa iliyokuwa mji pekee wa kujitegemea kati ya miji yote ya Uswahilini.

Visiwa vya Unguja na Pemba vilikuwa chini ya Omani tangu mwaka 1689, Wareno walipofukuzwa katika pwani za Uswahilini. 

Waananchi kuanzisha chama

Mwaka 1934, baada ya muda mrefu wa utawala wa Waraabu, wananchi wazalendo walianzishwa chama cha African Association (AA) kilichodhamiria kupinga ubaguzi dhidi ya watu wa Zanzibar.

Hususani chama hiki kilidhamiria kutafuta haki ya wakulima hasa wa karafuu, wanachama wa chama hiki walifanya kazi hiyo ngumu ya kutafuta haki kupitia matamasha ya michezo na sanaa.

Mwaka 1939 jamii ya washirazi walianzisha chama chao Shirazi Association (SA) kwa madhumuni ya kulinda na kutetea haki za jamii hiyo ya wanashirazi. 

Mwaka 1948 chama cha African Association kilibadilishwa jina na kuitwa Zanzibar African Association (ZAA). Baada ya mabadaliko haya, chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP), kilianzishwa kikiwa kimebeba maslahi mapana ya jamii wenye asili za Kiarabu, kuanzia hapa historia ya Zanzibar ikawa mweleko tofauti.

Mwaka 1957, vyama vya Zanzibar African Association (ZAA) na Shirazi Association (SA), viliamua kuunganisha nguvu kwa kuungana na ndipo kikazaliwa chama cha Afro Shirazi Party (ASP) mwenyekiti wake wa kwanza akiwa Shehe Abeid Amani Karume huku Katibu mkuu akiwa Shehe Thabit Kombo.

Chama cha Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP), kilizaliwa rasmi mwaka 1959 na waanzilishi wa chama hiki wakiwa ni Washirazi ambao hawakuridhia wala kukubali muunganiko wa ZAA na SA uliopelekea ASP kuzaliwa. 

Historia inaonesha kwamba baada ya muungano huo wa vyama huku vingine vikizaliwa, mwaka 1961 mwezi wa kwanza kulifanyika uchaguzi na vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo vilikuwa ni ASP, ZPPP na ZNP. 

Baada ya uchaguzi hakuna chama kilichopata kura za kutosha kuanzisha serikali. ASP walipata viti 10, ZNP viti 9 wakati ZPPP walipata viti 3, ambapo baadaye walipoteza kiti kimoja kilichokwenda ASP hivyo kukifanya kuwa na jumla ya viti 11.

Kwa tafsiri sahihi vyama vya ZNP na ZPPP ambavyo pia vilikuwa vinapigania kuunda serikali vilikuwa na viti 11 dhidi ya 11 vya ASP.

Baada ya pande hizo mbili kulingana, uchaguzi uliitishwa upya mwezi wa sita mwaka, 1961, awamu hii matokeo yalibadilika na ASP ikipata viti 10, ZNP viti 10 na ZPPP wakipata viti 3, hii ikaleta jumla ya kura 13 ya vyama viwili dhidi ya 10 vyya chama cha ASP. Kwa matokeo hayo ZNP na ZPPP wakapata ridhaa ya kuunda serikali ya Zanzibar.

Uchaguzi mwingine ukafanyika mwezi wa 7, mwaka 1963. Safari hii viti vikaongezwa, matokeo yalipotangazwa ASP walipata viti 13, ZPPP walipata viti 6, na ZNP wakapata viti 12, ikawapa jumla ya viti 19 dhidi ya viti 13 vya ASP hivyo ZNP na ZPP6P wakaendelea kusalia madarakani kwa uhalali wa hayo matokeo.

Uhuru bandia

Tarehe 10 Desemba 1963, Zanzibar ilitangazwa kuwa nchi huru na Waingereza lakini ikiwa chini ya Sultan Jeshmid bin Abdallah Al Said, na Waziri Mkuu akawa Mohamed Shamte. 

Uhuru huu wa bendera haukuwapendeza wafuasi wa Afro Shirazi Party (ASP), ambapo wengi wa wanachama wake walikuwa waafrika kwani kwa upande wa ZNP na ZPPP, wengi walikuwa ni waarabu, wazungu na wahindi. 

Hivyo iliaminika kuwa uhuru ule haukuwa kwa ajili ya wanyonge kwa maana ya wakulima na wakati kwenye mashamba kulikuwa na unyonywaji mkubwa na ukandamizwaji.

Wafuasi wa ASP waliudhika zaidi pia kutokana na ukweli kwamba nyakati zote za uchaguzi kulikuwa na hujuma dhidi ya ASP, walikuwa na uhakika wa kushinda lakini wakawa wanahujumiwa.

Kutokana na kutoridhika huko waliamua kuunganisha nguvu zao kupitia vikundi mbalimbali, vijana jasiri kama Seif Bakari, Kopa Omar (baba mzazi wa mwanamuziki wa taarabu Khadija Kopa) na wanamapinduzi shupavu, akiwemo John Okello, ambaye kwa asili alikuwa raia wa Uganda, kuipindua serikali iliyokuwa madarakani.

Liwalo na liwe

Ilikuwa ni usiku wa tarehe 12, Januari 1964, kundi la watu 300 waliposema liwalo na liwe, wakafanya mapinduzi, ikiwa ni siku 33 tu toka Uingereza itoe uhuru ‘bandia’ kwa Zanzibar. 

Zipo taarifa zinazoonesha kwamba watu waliokufa katika mapigano ni takribani 80 kwani mapinduzi yalilenga kuhakikisha damu nyingi haimwagiki kadri inavyowezekana.

Baada ya mapinduzi, Sultani Jeshmid nae alitoroka Zanzibar kwenda Dar es Salaam, ambapo kwa taarifa zisizo rasmi alikaa siku mbili kabla ya kwenda Uingereza. 

Mapinduzi hayo sasa yaliwezesha Wazanzibar kujitawala kupitia uongozi wa Waafrika kwa maana ya chama chao cha ASP, kilichokuwa kinaongozwa na Abeid Aman Karume na kukomesha miaka 200 ya utawala wa Waarabu Zanzibar.

Mapinduzi yatambuliwa

Baada ya mapinduzi, nchi zilizokuwa zinafuata ukomunisti wakati huo za China, Ujerumani Mashariki na Umoja wa Kisovyeti, zilikuwa za mwanzo mwanzo kuanzisha uhusiano wa kirafiki na serikali mpya ya Zanzibar kwa kuitambua rasmi na kwa kutuma washauri.

Baadaye Rais Karume alifanikisha majadiliano ya kuunganisha Zanzibar na Tanganyika ili kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.