Ijumaa , 20th Mei , 2022

Waziri wa TAMISEMI, Innocent Bashungwa, ameitaka sekta binafsi na washirika wa maendeleo kushirikiana na Serikali kuwatengenezea mazingira wezeshi wafanyabiashara wadogo  (Wamachinga) ili waweze kukuza biashara zao na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Waziri wa TAMISEMI, Mhe Innocent Bashungwa (Mb), akifungua warsha ya Wamachinga iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa ushirikiano na Mfuko wa Uendelezaji wa Sekta ya Fedha nchini (FSDT), jijini Dodoma.

Waziri Bashungwa ametoa rai hiyo jijini Dodoma wakati akifungua warsha ya Machinga iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa ushirikiano na Mfuko wa Uendelezaji wa Sekta ya Fedha nchini (FSDT).

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis, alisema kuwa shughuli za machinga zimesaidia kutatua changamoto za ajira kwa vijana kwa kujiajiri na kuwa sehemu ya ukuaji wa uchumi wa nchi.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Lawrence Mafuru, alisema kuwa Wizara yake ipo katika hatua za kutengeneza Bajeti Kuu ya Serikali, alisema miongoni mwa vipaumbele katika bajeti hiyo ambavyo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan angependa kuviona ni pamoja na sekta ambazo zinazalisha kama Kilimo, mifugo, uvuvi na nishati lakini pia wamachinga.

Mwenyekiti wa Wamachinga Taifa, Bw. Ernest Masanja, aliipongeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuwakutanisha na wakuu wa mikoa, makatibu tawala na wakuu wa wilaya kwa lengo la kutatua changamoto zao.

Kwa upande wa FSDT wameeleza kuwa wanafuraha kuunga mkono juhudi za ustawi wa wamachinga kwa kuwa ni sekta kubwa na inachangia asilimia 35 katika pato la Taifa.

Warsha hiyo imewakutanisha Makatibu Wakuu wa kisekta, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala, Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Idara, viongozi wa wamachinga na wadau wengine.