Jumatano , 16th Sep , 2020

Wafanyabiashara na wakulima wa kilimo cha mboga mboga jijini Dar es salaam wamesema changamoto kubwa inayowakabili ni upatikanaji wa mbegu bora pamoja na mbolea ya samadi wanayotumia.

Katika maeneo mbalimbali ya jiji pamekuwepo na watu wakijihusisha na biashara ya mboga za majani wengi wakilipa jina la kilimo cha Mjini ambapo hapa EATV imefika katika maeneo yao ya uzalishaji ili kuuona uhalisia ulivyo kwa Sasa katika biashara hiyo ambayo huchangia kwa kasi katika kuboresha afya ya mwili.

"Kusema ukweli mbegu ni tatizo pamoja na mbolea maana sisi tunaumia mbolea ya Samadi sio zile za dukani kwa iyo Kuna muda wafugaji wa kuku nao wanakuwa na uhaba hivyo tunapata shida,pia Niwaombe maafisa ugani watoke ofisini wawasaidie wakulima kujua kipi kinatakiwa Ili kuongeza mavuno" Mary Kibasa Mkulima wa mboga mboga.

Akizungumzia kilimo hicho bw Seif Mohamed wakati akifanya mahojiano amesema eneo hilo ni hifadhi ya barabara akiiomba serikali kuwapatia maeneo ambayo wanaweza kufanya kilimo hicho cha Mjini kwa kiasi kikubwa zaidi kwa kuwa hunufaisha watu wengi wakiwemo wauzaji wa mbolea,mbegu na mboga mboga kwa ujumla.

"Hapa tulipo tunalima kwa zaidi ya miaka 20 sasa lakini ni kwenye hifadhi ya barabara kwaiyo tungeomba serikali kama kuna maeneo ambayo wanahisi hajaendelezwa wangetupatia sisi tunafanya kilimo cha mjini kama hiki"alisema Seif Mohamed Mkulima wa mbogamboga.

Wamesema katika eneo hilo wao hutumia maji safi ya bomba kumwagilia mboga mboga hizo tofauti na watu wengi ambao wamekuwa wakisambaza uvumi kuwa walimaji wa kilimo cha mjini hutumia maji yasiyo salama kumwagilia wakiwasisitiza tuu maafisa ugani kutoka manispaa kuzidi kuhamasisha kilimo cha mjini.