Wafanyabiashara walia na wanasiasa maslahi uchumi

Jumatatu , 31st Aug , 2020

Wakati Tanzania ikielekea katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani Oktoba 28, wafanyabiashara wametaka viongozi watakaochaguliwa kusimamia sera ambazo zitakuza maslahi ya pamoja katika kukuza uchumi wa nchi.

Wafanyabiashara katika soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam

Wakizungumza na EATV Jijini Dar es Salaam wafanyabiashara hao wamesema licha ya kuwepo kwa sera katika kulinda masalahi ya wafanyabiashara ikiwemo kuondolewa kwa utitiri wa kodi wametaka sera zaidi ambazo zitamlinda mzalishaji wa ndani pamoja na kutenga masoko kulingana na aina za biashara.

"Ukweli changamoto kubwa sasa ni kupata soko la uhakika la bidhaa zetu wangetuwezesha kwa hilo ingesaidia zaidi waache kuangalia matumbo yao waongeze zaidi katika maslahi ya wananchi wote" amesema Mfanyabiashara wa Kariakoo Octavian Fabian

Kwa upande wao wadau wa biashara na uwekezaji wamesema bado wanamini kukua kwa uwekezaji kutokana na misingi ya amani na ushirikiano ambao umekuwepo huku wakisisitiza watakaopewa ridhaa ya kuongoza nchi kuendeleza sera bora za uwekezji nchini.

"Bado tunategemea uwekezaji kuimarika zaidi hatuna wasiwasi na hali ya kisiasa kwa sasa licha ya kuwepo kwa ushindani lakini katika eneo la uwekezaji bado tunaamini watakaopata nafasi za uongozi wataendeleza na kuboresha sera wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na wa nje ya nchi" amesema Moremi Marwa afisa mtendaji DSE