Jumamosi , 7th Mei , 2022

Tope lililopo katika soko la Mabibo Ndizi, Ubungo Jijini Dar es salaam limekuwa ni fursa kwa wakina mama mbalimbali wanaojishughulisha na kukodisha mabuti ya kutembelea kwenye tope na kuosha miguu ya watu wanaotoka sokoni humo.

Bi. Subira Simba, mjasiriamali anayewaosha miguu wanaofika soko la Mabibo

Baada ya tope kujaa ndani ya soko hilo maarufu Jijini Dar es salaam na kuzua wasiwasi kwa wafanyabiashara na watu wanaofika sokoni hapo kununua mahitaji ikiwemo matunda na chakula, wakina mama wanaokodisha mabuti ya kuvalia kwenye tope kwa wale wanaoingia sokoni humo pamoja na kuwaosha miguu wanaokuwa wametoka sokoni wanasema kipato wanachokipata kwa kazi hiyo ni kikubwa kiasi cha kuogopa kukitaja wazi kwani watu wote wanaweza kuacha kazi zao na kukimbilia hapo.

"Kwetu hili tope linatuingizia kipato. Mtu akitaka kuingia sokoni lazima akodi buti hapa kwa shilingi elfu moja, kama anashinda nalo ni elfu mbili. Lakini kama hawezi ataingia kisha wakati wa kutoka atakuja tutamuosha miguu kwa mia mbili. Aaah kwa siku ninaweza kukusanya elfu hamsini" - Subira Simba, Mjasiriamali katika soko la Mabibo Ndizi.

Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara katika soko hilo wameiambia EATV kwamba uwepo wa tope hilo katika soko lao kunawaathiri sana kibiashara kwakuwa hupoteza baadhi ya wateja wanaoshindwa kuingia sokoni huku kukiwa na tope.

"Kwakweli hapa tope linatutesa, hatupati faida kama inavyopaswa kuwa. Utanunua mzigo wa laki mbili lakini kwakuwa hakuna wateja wanaoweza kukanyaga tope unajikuta unakaa nao hata siku mbili, mfano ndizi zinakuwa zimeshaiva, ni hasara" - Ruthi Shayo, Mfanyabiashara.

Aidha, Swadaka Magesa ambaye ni Katibu Mkuu wa soko hilo amekili kuwepo kwa hali ya tope katika soko lake na kuiomba serikali iwasaidie kujenga miundombinu katika soko hilo ambalo lina wafanyabiashara wengi ili liweze kuwa na hali nzuri kama yalivyo masoko mengine katika Jiji la Dar es salaam.