Mkurugenzi wa Benki ya NCBA atembelea IPP Media

Ijumaa , 4th Sep , 2020

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NCBA Margaret Karume, ametembelea ofisi za IPP Media kwa lengo la kujionea namna gani vyombo vyake vya ITV, Radio One, Capital Radio na TV, EATV & EA Radio na The Guardian vinavyofanya kazi zake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NCBA Margaret Karume

Mkurugenzi huo amefika katika ofisi hizo hii leo Septemba 4, 2020, akiongozana na watendaji wake na kuvipongeza vyombo hivyo kwa namna vinavyogusa jamii kwa ujumla hususani akina  mama na vijana ambao ni sehemu kubwa ya jamii.

"Nimekuwa kwenye ziara hapa IPP Media, nimetembelea kitengo cha uandishi wa habari, cha uchapishaji, nimetembelea Radio na TV operesheni zake zinavutia sana, wakati unaingia katikati unakutana na mazingira mazuri ya kitaalamu kadri unavyozidi kwenda kwenye studio unapata kuona yanayojiri katika kuandaa habari”, amesema Margaret Karume

Aidha Margaret amesema kitu kinachovutia zaidi katika vyombo vya habari vya IPP ni huduma wanazotoa kwa vijana ,wanawake na wafanyabiashara ambazo zinaendana na kauli mbiu ya Benki ya NCBA.

“Kitu cha kuvutia zaidi IPP Media ni kuwa na studio nyingi na wanauwezo wa kuwahudumia vijana, wanawake na wafanyabiashara, hii ni hadithi moja inayoashiria ukuu na inaenda na kauli mbiu ya benki ya NCBA” amesema Margaret Karume.

"Nimebahatika kukutana na wafanyakazi wakarimu sana na angalau nimepata mwangaza wa kujua yale yanayojiri ili kupata habari tunazoziona kwenye Televisheni, nimeweza kuona jinsi gani magazeti yanachapishwa, nimepelekwa kwenye Radio na kuona jinsi habari zinavyoletwa pamoja", ameomgeza.