Ijumaa , 29th Apr , 2022

Mashirika ya ndege barani Afrika yameendelea kushuhudia ongezeko la idadi ya abiria huku nchi nyingi zikifungua uchumi wao baada ya miaka ya vikwazo vya Covid-19 ambavyo viliathiri vibaya sekta ya usafiri wa anga.

Ndege ya shirika la ATCL

Takwimu kutoka Jumuiya ya Kimataifa ya Usafiri wa Anga (IATA) na Muungano wa Mashirika ya Ndege ya Afrika (Afraa) zinaonyesha kuwa utendaji wa wasafirishaji wa kikanda umeimarika kwa asilimia 70 mwezi Februari na asilimia 69 kwa mwezi Machi 2022.

Kulingana na jumuiya hiyo, mapato ambayo mashirika ya ndege yalipata kwa Kilomita ya Mapato ya Abiria (RPK) yalikuwa juu ikilinganishwa na yale waliyopata mnamo Januari, na kuleta matumaini kwa tasnia ambayo iliathiriwa sana na kukatizwa na Covid-19.

"Mashirika ya ndege ya Afrika yalikuwa na ongezeko la asilimia 69.5 katika RPK za Februari dhidi ya mwaka mmoja uliopita, uboreshaji mkubwa ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 20.5 la mwaka hadi mwaka lililorekodiwa Januari 2022 na mwezi huo huo 2021" - IATA imesema.  

Shirika hilo linasema uwezo wa Februari 2022 uliongezeka kwa asilimia 34.7 na hii ni kwasababu mzigo ilipanda kutoka asilimia 12.9 hadi asilimia 63 hali inayoleta tumaini jipya kwa usafiri wa anga.  

Hata hivyo, kulingana na ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za serikali nchini Tanzania iliyowasilishwa mwanzoni mwa mwaka 2022, shirika la ndege la Tanzania limetajwa kuimarika huku usafirishaji wa mizigo ukionekana kuwa sababu ya afueni hiyo.