Madereva bajaj Manzese walia kukosa wateja

Alhamisi , 10th Sep , 2020

Umoja wa madereva wa Bajaji wanaotoa huduma ya usafiri kati ya Manzese na Mbezi wamesema wamekuwa wakikabiliwa na ugumu wa biashara kwa sasa kutokana na kuwepo kwa daladala zinazopita kubeba abiria kwa bei ya chini zaidi katika njia hiyo hali ambayo imekuwa ikiwaathiri kimapato.

Uongozi wa umoja huo pamoja wameieleza EATVĀ  kuwa daladala hizo ziliruhusiwa kubeba abiria na kuzunguka maeneo yote wakati wa kipindi cha corona, lakini hadi sasa zimeendelea kuwepo zikihatarisha ajira za vijana hao ambao walijikusanya kuunda umoja huo kama anavyoelezea Mwenyekiti na Katibu wa Umoja huo.

Aidha, wameiomba Manispaa husika ya Ubungo kitengo cha maendeleo ya jamii kushughulikia maombi ya mikopo yao kwa kuwa lengo lao lilikuwa kununua bajaji 20 ili ziweze kuwasaidia kuinua hali zao za Maisha tofauti na Bajaji za mkataba ambazo hupewa na mabosi zao.

"Kiukweli kwa sasa daladala za Manzese Mbezi zinatutesa sana zinafika hapa kituoni zinapakia kwa bei ndogo zaidi na zimekuja hapa tangu kipindi cha Covid 19 baada ya magari kuacha kutoa huduma nitumie fursa hii kuiomba serikali yetu kutuangali maana vijana wengi tuliwakusanya kutoka kwenye makundi ya mitaani".alisema mwenyekiti wa umoja huo.

Kwa upande wao baadhi ya madereva ambao ndio wahanga wa moja kwa moja wemesema shughuli hiyo kwa sasa ndio msingi wa kipato chao licha ya changamoto wanazopitia.