Jumatatu , 28th Sep , 2020

Baadhi ya wafanyabiashara wanaofyatua tofali na vifaa vingine vya kujengea vinavyotumia saruji Jijini Dar es Salaam wameiomba serikali kuingilia kati suala la kupanda kwa bei ya saruji kutoka shilingi 11,500 kwa mfuko mmoja hadi kufikia shilingi 15,000.

Eatv imefika eneo la Mbezi Tangi Bovu Jijini hapa na kuzungumza na wafanyabiashara wanaofyatua tofali eneo hilo ambao wameelezea kuyumba kwa bei ya saruji kunayumbisha biashara yao hali inayowalazimu kuongeza bei tofali kutoka 1,500 hadi 2000 kwa tofali moja hali inayoleta adha kubwa kwa wateja wao.

“Biashara kwa sasa imekuwa ngumu kiasi kutokana na kupanda kwa bei ya saruji, jambo ambalo limetulazimisha na sisi kupandisha bei ya tofali hadi kufikia 2000 huku wateja wetu wakilalamikia kushindwa kumudu bei hiyo,” alisema George Taimu muuzaji wa matofali.

Wafanyabiashara hao wa matofali wamesema bado hawajaelewa hasa sababu ya kupanda kwa bei ya saruji kwa kiasi hicho kwa sasa kiasi cha kuwa changamoto kwa shughuli yao hiyo inayowaingizia kipato na kuwaendeshea maisha yao.

“Hatujaelewa kwanini bei ya saruji imepanda kwa kiasi hiki kwa wakati huu, hali ambayo imeibua changamoto mpya kwa biashara yetu hii ambayo ndio tumekuwa tunaitegemea kwa kutuingizia kipato chetu,” alisema Steven Albert.

Biashara hii ya kuuza matofali mitaani imeajiri watu wengi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam ambao kwa sasa wamekuwa wakilalamikia upandaji wa bei ya saruji kuyumbisha biashara hiyo.