Friday , 24th Apr , 2015

Spika wa mabunge ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanakutana jijini Dar es Salaam leo, kujadili changamoto mbalimbali zinazozikabili nchi hizo ikiwemo tatizo la ugaidi ambalo hivi sasa linaonekana kushika kasi.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda.

Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda, ambaye ndiye mwenyekiti wa mkutano huo, amesema kuwa dhumuni kubwa ya mkutano huo ni kuona namna gani wanaweza kudhibiti matukio ya kigaidi.

“Hivi sasa kumekuwa matukio na matishio mengi ya kigaidi ndani ya Afrika Mashariki ambayo yanahitaji kupatiwa ufumbuzi, kwa mfano tukio la kusikitisha la kigaidi lililotokea hivi karibuni katika chuo kikuu cha Garisa na zaidi ya wanafunzi 100 kuuawa,” amesema.

Amesema wameona ni vema kukutana kama Jumuiya ili kushirikiana kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo kwa kuwa hakuna nchi yenye kinga ya mashambulio ya kigaidi.

Ameongeza kuwa mkutano huo ni wa 11, ambapo kila mwaka maspika wa nchi hizo hukutana mara mbili, ili kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo kutafutia ufumbuzi changamoto zinazozikabili nchi zao.

Vilevile spika hakusita kuzungumzia mambo muhimu yanayolikabili Taifa mwaka huu kuwa ni uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ikiwemo uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba ambapo Tanzania itajifunza namna nchi nyingine zilivyofanikiwa.

“Tulitarajia kupiga kura ya maoni Aprili 30 mwaka huu katika mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya, lakini shughuli hiyo haitafanyika kama ilivyopangwa, kutokana na kuchelewa kupatikana kwa mashine za kutosha za uandikishaji za BVR,” alisema.

Ameziomba nchi hizo jirani kuiombea Tanzania ili mwenyezi Mungu aepushe majanga yoyote yanayoweza kutokea na ivuke salama katika Uchaguzi huo Mkuu baadaye mwaka huu.

Spika Makinda amempongeza Spika Mpya wa bunge la Afrika Mashariki - EALA Bw. Daniel Kidega kutoka nchini Uganda, kwa kuchaguliwa kwake kuliongoza bunge hilo ambapo pia ndiye atakayekuwa mwenyeji wa mkutano wa 12 wa maspika utakaofanyika mwakani.

Spika wa Bunge la Uganda, Rebecca Kadaga, amesema wamekusudia kuweka mikakati ya muda mrefu itakayoleta ufumbuzi katika kutatua matatizo mbalimbali ikiwemo la ugaidi linaloukabili ukanda wa Afrika Mashariki.