Tuesday , 21st Apr , 2015

Watu wawili wameuawa katika matukio mawili tofauti likiwemo la kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni na mwingine kukutwa ametupwa huku akiwa ameuawa katika eneo la Kange jijini Tanga.

Mkuu wa Polisi nchini Tanzania, IGP Ernest Mangu.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa polisi Mkoa wa Tanga ZUBERI MWOMBEKI amesema mnamo tarehe 18/4/2015 majira ya saa nne asubuhi huko eneo la mapinduzi mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Mery Lucas (20) aliuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni na mtu aliyefahamika kwa jina la Khalfani Hamadi (46) mkazi wa mapinduzi jijini Tanga.

Kamanda Mwombeki amesema Marehemu alifariki wakati akiwa ameshafikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Bombo, ikiwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa kimapenzi na mtuhumiwa amekamtwa.

Na katika tukio la pili majira ya saa sita usiku wa kuamkia tarehe 20/4/2015 huko katika eneo la Kange jijini Tanga mtu mmoja ambaye hakufahamika jina, akiwa na jinsia ya kiume anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 30-35 alikutwa akiwa ameuawa na watu wasiojulikana, uchunguzi juu ya tukio hilo bado unaendelea.

Jeshi la polisi mkoa wa Tanga linatoa rai kwa wakazi wa jiji la Tanga kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu wanaoishi katika maeneo yao.