Sunday , 11th Jan , 2026

Tayari taarifa zilipelekwa Kituo cha Polisi na hatua zinaendelea pia Maafisa Ustawi wa Jamii wako sambamba na hatua husika.

Kufuatia kusambaa kwa taarifa za tukio la ukatili dhidi ya mtoto linalodaiwa kutokea eneo la Kinyerezi, Zimbili Mtipesa au karibu na Msikiti wa Mzee Uranga, Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema Serikali imeanza kuchukua hatua baada ya taarifa kupelekwa Kituo cha Polisi huku Ustawi wa Jamii na viongozi wote wa mkoa wa Dar es Salaam na Manispaa ya Ilala wakilifuatilia suala hilo kwa kina.

Kupitia chapisho aliloliweka kwenye ukurasa wake wa Instagram leo Januari 11, Dkt. Gwajima amewashukuru wale waliotoa taarifa kuhusu ukatili huo na kubainisha kuwa ukatili dhidi ya watoto ni jambo lisilokubalika na kwamba Serikali, kwa kushirikiana na jamii, imejipanga kukomesha vitendo hivyo.

“Ahsanteni wote mliotoa taarifa kuhusu ukatili huu mbaya kwa mtoto unaodaiwa kutokea huko Kinyerezi, Zimbili Mtipesa au karibu na Msikiti wa Mzee Uranga, Manispaa ya Ilala, mkoani Dar es Salaam.

Tayari taarifa zilipelekwa Kituo cha Polisi na hatua zinaendelea pia Maafisa Ustawi wa Jamii wako sambamba na hatua husika. Aidha, pia viongozi wote wa mkoa wa Dar es Salaam na Manispaa ya Ilala wako sambamba kwenye ufuatiliaji wa kina.” Amebainisha.

Aidha, Dkt. Gwajima ametoa wito kwa jamii kuwa na utulivu wakati Serikali ikiendelea kukusanya na kuandaa taarifa kamili kwa ajili ya umma akiomba pia kutafutwa kwa mama mzazi wa mtoto aliyekatiliwa, akimtaka awasiliane naye haraka kupitia namba ya simu 0765 345777.

“Ukatili kwa watoto hakika tutaukomesha wenyewe jamii kwa ushirikiano wetu kama hivi tunapeana taarifa mapema za watu katili kwa watoto ambao wao raha yao kukatili katili tu watoto na pia tutaukomesha kwa kuyaibua matukio ya ukatili na kutoa taarifa kama hivi sambamba na kuelimishana juu ya kuacha fikra za ukatili.” Ameongeza Dkt. Gwajima.

Kufuatia tukio hili ambalo lilisambaa jana Januari 10 likionesha picha mjongeo za mtoto huyo akifanyiwa ukatili, Dkt. Gwajima amesisitiza kuwa kila anayehusika na ukatili dhidi ya watoto atachukuliwa hatua kali za kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto.