Monday , 29th Dec , 2025

Akiwa katika ziara hiyo leo Desemba 29, 2025, Dkt. Mwigulu amesema kuwa ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji unaotokana na mabadiliko ya tabia nchi, Serikali ilianza utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amekagua hali za uzalishaji na usambazaji wa maji eneo la Ruvu Chini, mkoani Pwani na kuiagiza Wizara ya Maji ihakikishe suala la ukamilishaji wa mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda kupewa kipaumbele ili kukabiliana na upungufu wa maji.

Akiwa katika ziara hiyo leo Desemba 29, 2025, Dkt. Mwigulu amesema kuwa ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji unaotokana na mabadiliko ya tabia nchi, Serikali ilianza utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kwani maji ni uhai na hayana mbadala.

Waziri Mkuu ameagiza pia kukamilika kwa haraka usanifu wa mradi wa kutoa maji Mto Rufiji ambao ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2025/2030 ambayo inaielekeza Serikali kuanzisha Gridi ya Taifa ya Maji kwa kutumia vyanzo vikubwa vya maji kama Ziwa Victoria, Nyasa na Tanganyika.

Gridi hiyo itaenda kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa matumizi ya nyumbani pia mengine kwa ajili ya mifugo na shughuli za umwagiliaji ambapo mradi mkubwa utakuwa wa bomba kutoka Ziwa Victoria hadi mkoani Dodoma likipita mkoani Singida likiwa na njia mbili ya maji ya kunywa na ya kilimo na mifugo.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji katika kipindi cha muda mrefu, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ukamilishaji wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda wenye gharama ya shilingi bilioni 336, utekelezaji wake umefika asilimia 40.

Waziri Aweso ameongeza kuwa miradi mingine inayoendelea kutekelezwa pamoja kutoa maji Mto Rufiji eneo la Mloka kwa lengo la kuhakikisha DAWASA inakua na maji ya kutosha na kuanza utekelezaji wa mradi wa Kimbiji awamu ya pili.