Thursday , 18th Dec , 2025

“Jeshi la Polisi halitaruhusu watu binafsi au viongozi wa aina yoyote kuwatapeli wananchi kwa kisingizio cha matambiko au imani za kishirikina. Tuko tayari kulinda raia na mali zao wakati wote,”

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limetangaza  msimamo  mkali dhidi ya watu wanaojulikana kama "kamchape"" wanaojihusisha na vitendo vya kutapeli wananchi wakidai wanauwezo wa kufukuza wachawi na kuondoa vitu vibaya vinavyokwamisha Maendeleo ya wananchi.

Watu hao wamekuwa wakijipatia fedha kwa njia inayotajwa kuwa sio halali Kwa mujibu wa Sheria za nchi, ambapo wamekuwa wakichangisha fedha kutoka kwa nwananchi wakidai wanakamata wachawi na kuondoa vitu vibaya vikiwemo vya kishirikina vilivyowekwa na wachawi ili kukwamisha maendeleo ya wananchi.

Jeshi la polisi mkoani humo limeanza msako mkali wa kuwasaka watu hao ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao huku likiwatahadharisha wananchi kuachana na imani potofu ikiwemo kuamini ushirikina unaochochea mauaji, ukatili na vitendo vingine vya uhalifu.

Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Bwisya, Kisiwa cha Ukara, Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, kwa lengo la kutoa elimu ya usalama na kuhimiza utunzaji wa amani.

Akizungumza mbele ya viongozi wa Serikali, dini pamoja na wananchi, DCP Mutafungwa amesema jukumu la kulinda amani na usalama ni la kila mwananchi, akisisitiza kuwa hakuna mtu au kundi lolote litakaloruhusiwa kuvunja amani kwa kisingizio cha imani za kishirikina.

Amesema watu wanaojiita wataalam wa kusaka wachawi (Kamchape) wamekuwa wakijihusisha na uporaji wa mali, utapeli kupitia ramli chonganishi na kuvamia nyumba za wananchi kwa madai ya kuondoa uchawi, hali inayochochea chuki, hofu na uvunjifu wa sheria.

“Jeshi la Polisi halitaruhusu watu binafsi au viongozi wa aina yoyote kuwatapeli wananchi kwa kisingizio cha matambiko au imani za kishirikina. Tuko tayari kulinda raia na mali zao wakati wote,” amesema DCP Mutafungwa.

Kamanda Mutafungwa amewataka wananchi kuacha kuwahifadhi wahalifu hao, badala yake watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Aidha, amesema jumla ya watu 21 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo hivyo vya kihalifu, huku uchunguzi ukiendelea na mara utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

Kwa upande wao, baadhi ya wakazi wa Kisiwa cha Ukara akiwemo Maritha Nyangeta na Samsoni Ibrahim, wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa kufika kisiwani hapo na kutoa elimu ya usalama, wakisema hatua hiyo imewaondolea hofu waliyoishi nayo kwa zaidi ya miezi mitatu.

Wamesema kundi la Kamchape limekuwa likiwapita nyumba kwa nyumba, likiwatisha na kuwanyang’anya mali zao kwa madai ya kuwaondolea uchawi, hali iliyozua taharuki na kuathiri shughuli zao za kila siku.

Jeshi la Polisi limeahidi kuendelea na msako mkali dhidi ya watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo hadi vitakapotokomezwa kabisa.