Wednesday , 22nd Oct , 2025

“Kama Chama tunajipanga kuagiza Mawakili waliopo Mara na Mwanza ili waelekee huko kutoa huduma za kisheria kwa Heche”

Kufuatia taarifa iliyotolewa na Katibu mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Mnyika juu ya Makamu mwenyekiti wa Chama hicho John Heche, kukamatwa na polisi katika geti la kuingilia katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam leo Oktoba 22, 2025, Mkurugenzi wa Sheria wa CHADEMA, Gaston Garubindi amesema Heche amesafirishwa mchana huu kwenda Tarime.

akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya kutoka kufuatilia kukamatwa kwa John Heche, Gaston amesema baada ya kufika Polisi wameambiwa tayari Heche hayupo Dar es Salaam na amesafirishwa Kwenda Tarime mkoani Mara.

“Heche ambaye asubuhi alikamatwa Mahakamani na Polisi, taarifa ya Polisi inasema kweli wamemkamata kwa makosa ambayo hawajayasema lakini anasema jambo la Heche halipo Dar es salaam lipo Tarime na anadai tayari wamemsafirisha Heche kutoka Dar kwenda Tarime”

“Kama Chama tunajipanga kuagiza Mawakili waliopo Mara na Mwanza ili waelekee huko kutoa huduma za kisheria kwa Heche” ameongeza.

Katika taarifa ya awali, Mnyika alisema Heche, amepelekwa katika Kituo Cha polisi Cha Central na kuongeza kuwa amesikitishwa na kitendo hicho akitoa rai kwa jeshi la polisi kutoa sababu ya kukamatwa kwake akilihusianisha tukio hilo na tukio la Heche kutaka kwenda kumzika Raila Odinga nchini Kenya lililozua mzozo katika mpaka wa Sirari siku chache zilizopita.