Friday , 4th Jul , 2025

Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi ametoa wito kwa watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kwa weledi, ufanisi na kuzingatia maadili kwani kwa kutofanya hivyo kumesababisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awe analalamikiwa na watanzania.

Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi ametoa wito kwa watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kwa weledi, ufanisi na kuzingatia maadili kwani kwa kutofanya hivyo kumesababisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awe analalamikiwa na watanzania.

Maswi ametoa wito huo leo Julai 3, 2025 alipokuwa akifunga rasmi mafunzo elekezi kwa wafanyakazi 79 kutoka Wizara ya Katiba na Sheria na Tume ya Haki za Binadamu yaliyofanyika kwa siku tatu katika ukumbi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere Kibaha, mkoani Pwani.

“Kumekuwa na changamoto kwetu sisi watumishi wa Umma ya utendaji kazi ulio dhaifu na maadili mabaya, jambo linalosababisha Rais alalamikiwe, niwaambie leo Rais akilalamikiwa yeye sio tatizo, tatizo ni sisi tuliopewa nafasi na kushindwa kutekeleza vizuri majukumu yetu, mkisimama imara serikali haitalaumiwa” alisema.

“Mafunzo haya mliyoyapata ni mwanzo mzuri wa utoaji huduma bora kwa watanzania kwa kuwa yametolewa kwa lengo la kuwajengea misingi thabiti, uelewa wa sheria, mbinu mpya za utendaji kazi, pamoja na namna ya kuilinda serikali ili kuhakikisha inaendeshwa kwa mujibu wa sheria” alisisitiza.  

Maswi aliongeza  kwa kuwataka watumishi wawe waaminifu kwa serikali, wafanye kazi kwa weledi, watumie vizuri muda wa kazi na kuzingatia maadili ya kazi ikiwa ni pamoja na kujiepusha na rushwa, ufisadi, kutunza siri na taarifa za serikali, kuwahi kazini na kushirikiana kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi na kujenga uaminifu wao kwa serikali.

Aliongeza kuwa malalamiko mengi yanayosikika yanatokana na watumishi wa Umma kutokuwa na maadili kwa kuendekeza vitendo vya rushwa, ufisadi, utovu wa nidhamu, kukosa ushirikiano pamoja na kutotambua haki za serikali jambo linaloathiri ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi, kuongeza gharama kwa serikali pamoja na kuharibu taswira ya taasisi kwa maana ya Wizara.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utawala na Rasilimali watu kutoka tume ya Haki za Binadamu, Gabriel Rhobi alitoa shukrani zake za dhati kwa Katibu Mkuu kwa kuruhusu na kutoa fedha ili mafunzo hayo yafanyike na kusema kuwa mafunzo hayo yamewajengea uwezo washiriki wote na tayari ameona mabadiliko katika upande wa maadili hasa mavazi.

Mwenyekiti wa mafunzo hayo Evarist Mashima kutoka Wizara ya Katiba na Sheria pia alimshukuru Katibu Mkuu kwa kuwezesha mafunzo haya kufanyika na kusema kuwa washiriki wameweza kujifunza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Muundo wa Wizara na namna majukumu yake, Mfumo wa uendeshaji Serikali na mgawanyo wa majukumu, maadili mema ya mtumishi wa Umma, Maandalizi ya kustafu, Sheria ya Utumishi wa Umma sura 298 inayoelezea wajibu na haki za mtumishi Pamoja na usalama serikalini kwa maana ya utunzaji wa siri za serikali.