Thursday , 19th Jun , 2025

Maafisa wawili wa polisi waliomshambulia na mmoja wao kumfyatulia risasi kijana aliyekuwa anauza barakoa siku ya maandamano ya kupinga mauaji ya kijana Albert Ojwang aliyefia mikononi mwa polisi nchini Kenya, wataendelea kuzuiliwa na polisi kwa siku 15 zaidi huku uchunguzi ukiendelea.

Askari wawili waliomfyatulia risasi muuza barako Kenya

Klinzy Masinde Barasa na Duncan Kiprono watazuiliwa katika kituo cha polisi cha Capitol Hill ili kuruhusu upande wa mashtaka kukamilisha uchunguzi wake.

Askari Polisi hao walikamatwa baada ya vídeo yao ya Juni 17, 2025, kusambaa mitandaoni ikionesha mmoja wao akimfyatulia risasi Boniface Kariuki wakati akijaribu kuondoka katika eneo hilo.

Kifo cha kutatanisha cha Albert Ojwang, aliyekuwa mwalimu ambaye alikamatwa na Polisi nchini humo kwa madai ya kuchapisha taarifa potofu katika mtandao wa X zamani Twitter na kisha baadaye kuuawa kwa kupigwa na kunyongwa na polisi akiwa rumande, kimesababisha maandamano katika maeneo mbalimbali nchini Kenya huku kukiwa na shinikizo la kuwataka waliohusika na mauaji hayo katika ngazi za juu za idara ya polisi nchini Kenya wawajibishwe.