Tuesday , 11th Mar , 2025

Polisi wa Ufilipino wamemkamata rais wa zamani Rodrigo Duterte baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kutoa hati inayomshutumu kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu kutokana na "vita vyake dhidi ya dawa za kulevya".

Mzee huyo mwenye umri wa miaka 79 aliwekwa chini ya ulinzi wa polisi muda mfupi baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Manila kutoka Hong Kong.

Hajaomba radhi kwa ukandamizaji wake wakati wa vita dhidi ya dawa za kulevya, ambao ulishuhudia maelfu ya watu wakiuawa alipokuwa rais wa taifa hilo la Kusini Mashariki mwa Asia kuanzia 2016 hadi 2022, na meya wa jiji la Davao kabla ya hapo.

Alipokamatwa, alihoji msingi wa hati hiyo, akiuliza: "Ni uhalifu gani nimefanya?
Msemaji wa zamani wa rais wa Duterte Salvador Panelo amelaani kukamatwa kwake na kusema kuwa ni "kinyume cha sheria" kwani Ufilipino ilijiondoa kutoka ICC mwaka 2019.

Hapo awali ICC ilisema kuwa ina mamlaka nchini Ufilipino kuhusu uhalifu unaodaiwa kufanywa kabla ya nchi hiyo kujiondoa kama mwanachama.

Lakini wanaharakati walitaja kukamatwa kwa "wakati wa kihistoria" kwa wale walioangamia katika vita vyake vya dawa za kulevya na familia zao, Muungano wa Kimataifa wa Haki za Kibinadamu nchini Ufilipino ulisema.
Duterte alikuwa Hong Kong kufanya kampeni kwa ajili ya uchaguzi ujao wa Mei 12 katikati mwa muhula, ambapo alikuwa amepanga kugombea umeya wa Davao.

Picha zilizorushwa kwenye runinga ya ndani zilimuonesha akitoka nje ya uwanja wa ndege akitumia fimbo. Mamlaka zinasema yuko "afya na njema" na anahudumiwa na madaktari wa serikali.

"Kosa langu ni nini? Nilifanya kila kitu kwa wakati wangu kwa ajili ya amani na maisha ya amani kwa watu wa Ufilipino," aliuambia umati wa wahamiaji wa Ufilipino kabla ya kuondoka Hong Kong.