Friday , 21st Feb , 2025

Wakaguzi na Askari wa Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha na Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo nchini waliofanya vizuri zaidi kazini mwaka 2024 wamehimizwa kuwa mabalozi wazuri lakini pia kuwa chachu ya mabadiliko katika utendaji wa kazi kwa askari wengine.

Wito huo umetolewa na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Simon Pasua leo Februari 21, 2025 wakati akitoa vyeti vya sifa na zawadi kwa Askari hao katika viwanja vya Kikosi cha Kutulizia Ghasia Arusha (FFU Oljoro).

Kamanda Pasua amebainisha kuwa Jeshi la Polisi limekua na utaratibu wa kuwatambua na kuwapongeza Askari wake waliofanya vizuri ili kuongeza ari na hamasa katika utendaji wa kazi, hivyo wakaguzi na askari waliofanya vizuri wamesisitizwa kuendelea kufanya kazi kwa nidhamu ili kuwa mfano mzuri kwa Askari wengine.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamzi wa Polisi SACP Justine Masejo pamoja na kuwapongeza askari hao, amewataka kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia nidhamu, kutenda haki, weledi, kuwa waadilifu na kutoa huduma bora kwa wananchi.

SACP Masejo amesema zawadi hizo zimetolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi huku akibainisha kuwa askari wote wamefanya vizuri, ila waliopewa zawadi ni wawakilishi kutoka kila eneo la utendaji kazi ambao wamefanya kazi vizuri zaidi kwa kujituma na kushirikiana na askari wenzao katika kuwahudumia wananchi.

Naye Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Abel Paul ambaye ni miongoni mwa askari 14 waliopongezwa, ameushukuru uongozi mzima wa Jeshi hilo kwa kutambua utendaji wao wa kazi na kubainisha kuwa zawadi hiyo imetokana na ushirikiano mzuri toka kwa askari wengine katika utekelezaji wa majukumu yao huku akisema zawadi hiyo itaongeza hari na ufanisi katika utendaji kazi.